Na: Amina Mambo Wananchi wametakiwa kufahamu kuwa kitendo cha kupatwa kwa mwezi hakitakuwa na madhara yoyote kwa binadamu bali tulio hilo litapelekea nuru ya mwezi kuonekana kuwa na giza kwa kuwa kupatwa kwa mwezi hutokea kipindi mwezi ukiwa mbali na dunia tofauti na walivyozoea.
Akizungumza na SUAMEDIA ofisini kwake Kaimu Meneja Msaidizi Mamlaka ya Hali ya Hewa Kanda ya Mashariki TMA Morogoro, Bw. Kasian Livangala amesema kuwa, tukio hilo la kupatwa kwa mwezi linatarajia kutokea leo saa nne na nusu usiku na litaendelea hadi saa sita na robo usiku.
“Siku ya ijumaa usiku wa tarehe 27 julay 2018, tukio la kupatwa kwa mwezi linatarajiwa ambapo nuru ya mwezi mkamilifu itazuiwa na Dunia hivyo mwezi kuonekana kuwa na rangi myekundu katika kipindi cha masaa kadhaa kuanzia saa 4.30 usiku hadi saa 6.14 usiku.”amesema Livangala. Kaimu Meneja Msaidizi Mamlaka ya Hali ya hewa Kanda ya Afrika Mashariki (TMA) Morogoro, Cassian Livangala akitoa maelezo kuhusiana na kupatwa kwa mwezi tarehe 27/07/2018 ofisini kwake.(Picha na Amina Mambo)
Bw. Livangala ameongeza kuwa kutokana na umbali mkubwa kati ya mwezi na dunia hali ya bahari kujaa na bahari kupwa haitarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa na pia hakuna mabadiliko makubwa ya hali ya hewa yanayotarajia kutokea katika tukio hilo.
“Kwa vile katika tukio hili mabadiliko katika nguvu za uvutano kati ya Dunia na mwezi yatakuwa ni madogo kutokana na umbali mkubwa kati ya mwezi na dunia hali ya Bahari kujaa na Bahari kupwa haitarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa na pia hakuna mabadiliko makubwa yanayotarajiwa katika mifumo ya hali ya hewa”amesema Livangala.
Aidha Bw Livangala amesema kuwa tukio la kupatwa kwa mwezi linatarajiwa kuonekana vizuri katika maeneo mengi ya bara la Afrika, Asia na Ulaya huku nchini Tanzania tukio hilo linatarajiwa kuonekana katika maeneo mengi na kuongeza kuwa litaonekana kwa muda mrefu zaidi ukilinganisha na matukio mengine katika karne ya 21.
|