Na Gerald Lwomile
Dar Es Salaam
Maonesho ya Vyuo Vikuu nchini yameanza rasmi leo Julai 26, 2021 na yanatarajiwa kufikia tamati ifikapo Julai 31, 2021 ambapo wanafunzi mbalimbali wanatarajiwa kupata nafasi ya kufanya udahili wa kujiunga na masomo ya elimu ya juu nchini
Wanafunzi wanaotarajiwa wa kujiunga na Vyuo Vikuu nchini wakiwa katika Banda la SUA ili kupata maelezo ya namna ya kufanya Udahili
Kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) maonesho hayo ya Vyuo Vikuu nchini yanatarajiwa kufunguliwa rasmi Julai 27 na Katibu Mkuu Kiongozii wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Zena Ahmed
Akizungumza katika Banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Mratibu wa Maonesho hayo kwa upande wa SUA na Msimamizi wa Kitengo cha Ugani Dkt. Innocent Babili amesema SUA imejipanga kuhakikisha inawasaidia wanafunzi kudahili ili wapate nafasi ya kujiunga na masomo chuoni hapo
Dkt. Babili akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la SUA
Dkt. Babili amesema tayari wanafunzi mbalimbali wameanza kufika katika Banda la SUA kwa ajili ya kupata ushauri na namna sahihi ya kuchagua kozi za kusoma ambazo zinatolewa zaidi katika Kampasi tatu za chuo hicho ambazo ni Kampasi ya Edward Moringe zamani ikijulikana kama Kampasi Kuu, Solomon Mahlangu na Kampasi mpya ya Mizengo Pinda iliyoko Mkoani Katavi
Katika hatua nyingine Dkt. Babili amewataka watu wote ambao hutumia fursa ya maonesho ili kujipatia mahitaji mengine kama miche ya matunda na mbogamboga kwenda kununua miche hiyo SUA badala ya kuifuata kwenye maonesho jambo linaloweza kuleta msongamono na kupelekea kuwepo kwa hatari ya maambukizi ya COVID 19
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) tayari imefungua dirisha la udahili tangu tarehe 12 Julai, 2021 na imewaomba pia watu kuhudhuria maonesho ya 16 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia huku wakichukua tahadhari za ugonjwa wa CORONA kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni na kuepuka misongamano wawapo eneo la tukio