Na: Bujaga I. Kadago Watanzania wamehakikishiwa kupokea wahitimu wa Chuo Kikuu katika fani za Kilimo walioiva kwa nadharia na vitendo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kufuatia kupatiwa matrekta na zana zake kamili kumi kulingana na ahadi ya Rais Dr. John Pombe Magufuli.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, (SUA) Prof. Raphael Chibunda alipokuwa akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa matreka hayo kumi ya ahadi ya Rais Wa Tanzania hafla iliyofanyika katika kiwanda cha Tamco Kibaha Mkoa wa Pwani. Aidha Prof Chibunda amelihakikishia Shirika la Maendeleo la Taifa NDC kuwa SUA iko tayari kuwa kituo cha mafunzo kwa matrekta haya kwa ajili ya Mkoa wa Morogoro ambapo amesema eneo la kituo liko tayari na sasa wako tayari kuanza utekelezaji huo. Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa NDC Prof. Damian Gabagambi alisema nchi bado inahitaji zaidi zana za kilimo ili kweli wakulima wa Tanzania wageukie katika kilimo cha kisasa na endelevu na kwa sasa kupitia mradi huu wa matrekta wamejipanga kutoa mafunzo kwa madereva wote wa matrekta yatakayonunuliwa lakini pia yatahudumia matengenezo kwa mwaka mmoja.
|