Na Gerald Lwomile
Dar Es Salaam
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekimwagia sifa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuanzisha kozi ambazo zitasaidia kukuza uchumi wa nchi kwa kupika wataalamu ambao watasambaza maarifa na ujuzi kwa wakulima lakini pia wataalamu ambao wanauwezo wa kujiajiri wenyewe.
Afisa kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshugulikia elimu ya juu Bw. Clement Sanga akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Udahili SUA Bi. Anitha Ngesi juu ya kozi mpya, kushoto ni Mratibu wa Maonesho na Mkuu wa kitengo cha ugani SUA Dkt. Innocent Babili
Akizungumza na SUA Media, Afisa kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshugulikia elimu ya juu Bw. Clement Sanga amesema SUA imeangalia mbali sana kwa kuanzisha kozi kama ya Rasimali Nyuki na Mazao yake pamoja na kozi ya Uwekezaji katika Kilimo na Huduma za Kibenki.
“Kozi kama hii ya Shahada ya Rasimali Nyuki na Mazao yake itamwezesha mwanafunzi kupata ujuzi wa kutosha katika elimu kuhusu Nyuki na namna ya kuzalisha mazao yatokanayo na nyuki kwa ubora utakaosaidia kuinua uchumi wa nchi”, amesema Sanga
Akizungumzia kozi ya Uwekezaji katika Kilimo na Huduma za Kibenki ambayo ni moja ya kozi mpya SUA, Bw. Sanga amesema kwa muda mrefu wakulima nchini wamekuwa hawapewi kipaumbele katika mikopo kutokana na kukosekana kwa maarifa na ujuzi wa uwekezaji katika miradi ya kilimo
Amesema, wataalamu katika kozi hii watakuwa na ujuzi katika uwekezeji katika kilimo na wanaojua vizuri mambo ya benki na hivyo watasaidia katika kukuza sekta ya kilimo ambayo huajiri watu wengi nchini. Hivyo, kozi hiyo itasaidia wakulima kupata huduma za wataalam husika kupata mikopo ya benki ambapo tofauti na sasa wakulima wengi hawapati mikopo kwa kiwango cha kutosha
Naye Ali Saidi na Magreat Senganywa ambao ni miongoni mwa wadau waliotembelea banda la SUA wameiambia SUA Media kuwa kozi zinazotolewa na SUA ni za kipekee na zinaweza kumsaidia mwanafunzi kuajiriwa na kujiajiri katika sekta ambayo amesomea. Pia humwandaa na kumuimarisha mwanafunzi kukabiliana na changamoto mbalimbali katika shughuli za kila siku.
“Kusoma kilimo kunaweza kukusaidia kujua mambo mbalimbali kwani hivi sasa hakuna kitu kinaweza kwenda bila kuwa na kilimo cha uhakika kwani kilimo ndiyo kinatupa chakula, mavazi na hata kuinua Maisha yetu” amesema Saidi.
Maonesho ya Vyuo Vikuu yanaendelea huku yakitarajiwa kufungwa rasmi tarehe 31 Julai, 2021 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Prof. Joyce Ndalichako.