Na: Gerald Lwomile Serikali imezitaka Mamlaka zinazoshughulika na kutoa vibali mbalimbali kwa wajasilimali nchini kuhakikisha wanatoa maelekezo ya namna ya kupata vibali hivyo badala ya kuwafungia kutofanya biashara.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mh. Charles Mwijage Agosti 4 wakati akifungua maonesho ya 25 ya Kilimo Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere mkoani Morogoro. Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda akitoa zawadi inayofahamika kama Shangazi Kaja SUAMEDIA kwa mgeni rasmi Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mh. Charles Mwijage alipotembelea banda la SUA. (Picha na Tatyana Celestine)
Mh. Mwijage amesema kuwa wakati mwingine imekuwa ikishangaza kuwa mamlaka za Serikali ambazo zingeweza kuwasaidia wajasiliamali na hasa wasindikaji wa mazao yatokanayo na kilimo kuwafungia badala ya kusaidiwa.
Amesisitiza kuwa katika kuhakikisha wajasilimali wasindikaji wanasaidiwa upo umuhimu mkubwa kwa Shirika la Viwango Tanzania TBS, Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA na Taasisi zingine zinazohusika na utoaji wa vibali kuhakikisha vinawasaidia zaidi wajasiliamali hao wanaoanzisha viwanda. Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mh. Charles Mwijage aliyevaa skafu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mh. Kebwe Stephen Kebwe wakianza kutembelea Maonesho ya Nanenane. (Picha na Vedasto George)
Akizungumzia kuhusu kuinua pato la mtanzania Mh. Mwijage amesema kuwa Serikali inafanya jitihada za makusudi katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda na kuwataka watanzania kuwekeza katika viwanda ili kujenga uchumi wa kati ifikapo 2025.
|”Uchumi wa kitaifa ni zaidi ya uchumi wa taifa,…, ifikapo 2025 tujenge uchumi wa kitaifa, uchumi wa taifa zima ambao ni uchumi jumuishi, tungependa kufika wakati huo na tutafika wakati huo au kabla ya hapo wastani wa kipato cha mtanzania kikiwa dola elfu 3 ambazo ni sawa na shilingi milioni 7 na nusu” amesema Mh. Charles Mwijage. Kikapu maarufu kama Shangazi Kaja kilichoandaliwa na SUAMEDIA kimesheheni bidhaa za mbogamboga na matunda zilizotolewa na Idara ya Sayansi ya Mimea na Kilimo cha Bustani. (Picha na Tatyana Celestine)
Amesema kuwa kama watanzania watalima kilimo chenye tija nchi nzima, kipato cha mtanzania mmoja mmoja kitaongezeka na kufikia hadi milioni 7 na nusu kwa mwaka.
Awali akitembelea banda la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Mh. Mwijage amewapa changamoto watafiti wa SUA kuhakikisha Teknolojia za kilimo na tafiti zinawafikia wananchi ili kuinua kilimo nchini.
Ametolea mfano wa ng’ombe wa mataifa mengine kama Saudi Arabia ambapo ng’ombe hutoa hadi lita 60 za maziwa wakati ng’ombe wa Tanzania huishia lita 20 tu za maziwa na kuwataka watafiti kuhakikisha wanafata utafiti utakaowezesha ng’ombe kutoa angalau lita 50 ili kuinua pato la mkulima.
Aidha Mh. Mwijage amewapongeza SUA kwa kazi mzuri wanayoifanya, Maonesho ya Nanenane 2018 yamefunguliwa rasmi Agosti 4 na yanatarajiwa kuendelea hadi Agosti 8 yatakapofikia kilele chake. |