Na Gerald Lwomile
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimesema mjadala ulioendeshwa na Watafiti kutoka chuoni hapo na kushirikisha wadau mbalimbali wenye mada isemayo “Kilimo Ikolojia na Mifumo ya Chakula nchini Tanzania” kwa kiasi kikubwa itasaidia kutoa uelewa juu ya janga la uhaba wa chakula ambalo linatarajiwa kuwa kubwa Zaidi ifikapo mwaka 2030
Hayo yamesemwa na Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) upande wa Taaluma Prof. Maulid Mwatawala wakati akifungua mjadala huru uliowashirikisha wadau mbalimbali ukiwa umelenga kujadili kwa kina na kutoa mapendekezo juu ya Kilimo Ikolojia nchini
Prof. Mwatawala amesema ripoti ya Chakula na Lishe ya mwaka 2020 inaonesha kuwa Ulimwengu uko nyuma katika utekelezaji wa kutokomeza baa la njaa ifikapo mwaka 2030 na kuna sababu nyingi ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi na hivi sasa janga la ugonjwa wa COVID 19
“Mifumo ya vyakula inapitia katika kipindi kigumu na vikwazo mbalimbali vikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi na hivi karibuni changamoto ya ugonjwa wa COVID 19”, amesema Prof. Mwatawala
Amesema kuwa bara la Asia, Afrika na Amerika ya Kusini yameathirika Zaidi na upungufu wa chakula kwani karibu watu bilioni mbili wanatoka katika Mabara hayo huku Tanzania katika wilaya 16 zimekuwa na watu waathirika wa chakula milioni 1 kati ya watu milioni 4.8
Naye Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mafunzo ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji Teknolojia na Ushauri wa Kitaalam Prof. Esron Karimuribo amesema SUA inayo Fahari kubwa katika kuhakikisha watafiti wake wanashiriki kikamilifu katika mijadala mbalimbali ya Umoja wa Mataifa ikiwemo mjadala huru wa mifumo ya chakula
Amesema lengo la Chuo ni kuhakikisha inatoa fursa katika mifumo hiyo ya chakula ili kupambana na uhaba wa chakula kwa kuhakikisha kunakuwa na usalama wa chakula nchini
Kwa upande Mratibu wa Mradi wa Kuvijengea Uwezo Vyuo Vikuu SUA Prof. Antony Sangeda amesema Mradi huo utaendelea kushirikiana na Mradi wa Kilimo Ikolojia ambapo pia kwa kushirikiana na Mradi huo wameanzisha Mtaala wa Kilimo Ikolojia ambapo tayari wanafunzi mbalimbali wameanza kuchukua fani hiyo katika ngazi ya Umahili
KATIKA VIDEO