Na Gerald Lwomile
Dar Es Salaam
Imeelezwa kuwa ili Tanzania iendelee kubaki katika Uchumi wa Kati, tafiti mbalimbali za kimataifa zimeonesha ni lazima nchi iwe na rasimali watu wenye elimu ya juu kwa asilimia 12 na ujuzi wa kati kwa asilimia 26 vinginevyo inashuka kiuchumi
Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zena Ahmed Said akifungua maonesho ya TCU 2021
Akizungumza Julai 27, 2021 katika ufunguzi wa Maonesho ya Vyuo Vikuu yanayoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu nchini Mgeni rasmi ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zena Ahmed Said amesema kutokana na tafiti hizo Tanzania haina budi kuhakikisha inakuwa na idadi hiyo ya rasimali watu ili kuinua uchumi wake
Mhandisi Zena amesema kwa tafiti za mwaka 2016 nchini Tanzania rasimali watu wenye elimu ya juu ni asilimia 3.3 huku wenye ujuzi wa kati ikiwa ni asilimia 17 tu jambo linalotengeneza tafsiri kuwa taasisi za elimu ya juu nchini bado zina kazi kubwa kuhakikisha zinazalisha rasimali iliyobaki ili kufikia malengo
“Wastani huu bado uko chini sana hivyo ni muhimu kuendelea kuweka mipango itakayoongeza idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu ili wapate ujuzi na maarifa yanayotakiwa sokoni”, amesema Mhandisi Zena
Amesema kuwa mkakati wa kitaifa wa kukuza ujuzi na maarifa ulioanza mwaka 2015 ni mkakati endelevu ambao ni muhimu sana kwa taifa ambao umefanya mengi kwa elimu ya juu na kati na kusisitiza kuwa ni vyema kuangalia nchi zingine zimefanikiwa vipi
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda aliyekaa katikati akiwa katika picha ya pamoja na waoneshaji kutoa SUA, kulia waliokaa ni Mkurugenzi wa Kurugenzi wa Shahada za Awali SUA Dkt. Nyambilila Amuri
Awali akimkaribisha mgeni rasmi kufungua maonesho hayo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe amesema kuwa maonesho ya TCU ni muhimu sana kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita lakini pia na wanafunzi kwa ujumla
Amesema umuhimu wa maonesho hayo ni pamoja na kumsaidia mwanafunzi wa kidato cha tano kuamua na kujiwekea malengo ya kuamua nini akifanye katika kuhakikisha anafikia ndoto zake
“Maonesho haya ni muhimu kwa ajili ya kujiandaa na mtihani wako wa kidato cha sita, ni wakati mzuri sasa wa kujua ni kitu gani hasa utaenda kusoma baada ya mtihani wako wa kidato cha sita na taasisi zetu zote za elimu ya juu ziko hapa” amesema Prof. Mdoe
Maonesho ya Vyuo Vikuu yanaendelea kwa kuingia siku ya tatu tarehe 28 Julai, 2021 na yanatajiwa kumalizika rasmi tarehe 31 Julai, 2021 mwaka huu, maonesho haya yamebeba kauli mbiu isemayo “Kuendeleza, Kukuza na Kudumisha Uchumi wa Kati kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia”
Mkurugenzi wa Kurugenzi za Shahada ya Awali Dkt. Nyambilila Amuri waliokaa katikati akiwa katika picha ya pamoja na waoneshaji kutoka SUA, kushoto waliokaa ni Mratibu wa maonesho kutoka SUA Dkt. Innocent Babili na kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko SUA Mariam Mwayela