Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kuwa mwenendo wa ugonjwa wa corona nchini humo huenda ukawa “mbaya zaid kabla ya hali kuimarika”, wakati alipofufua tena mkutano wake na wanahabari.
Bw. Trump pia ametoa wito kwa Wamarekani wote kuvalia barakoa, akisema kuwa “zitasaidia kudhibiti maambukizi” na kwamba ni ishara ya “uzalendo”.
Rais, hakua amevalia barakoa wakati akitoa maelezo kwa wanahabari, lakini aliwahi kupuuza suala la kuvaa kifaa kinga hicho.
Inasemekana wasaidizi wake wamemuasa kuchukua hatua zenye malengo wakati ambapo maambukizi yanazidi kuongezeka kote Marekani.
Utoaji taarifa kuhusu corona kwa vyombo vya habari kutoka Ikulu ya Marekani, mwisho ilikuwa Aprili punde tu baada ya Trump kusema kuwa virusi hivyo vinaweza kutibiwa kwa watu kujipaka dawa za kuua vijidudu.
Baada ya miezi kadhaa, taarifa yake ya Jumanne ambayo ilionekana kupangwa, rais aliashiria kuunga mkono kile ambacho maafisa wa afya wamekuwa wakisema kupitia jopo lake la kukabiliana na ugonjwa huo na kuonya kwamba: “Kwa bahati mbaya hali huenda ikawa mbaya zaidi kabla ya kuanza kubadilika.
“Wakati mwingine huenda sipendi kusema kuhusu mambo, lakini hivyo ndivyo ilivyo.”
Aliongeza: “Tunataka kila mmoja ikiwa atashindwa kutekeleza kanuni ya kutokaribiana, avae barakoa.
“Ama uwe unapenda barakoa au la, zina machango wake, zitakuwa na athari yake na tunahitaji kila kitu tunachoweza kupata.”
Bwana Trump – ambaye zaidi ya mara moja alirejelea kuwa ugonjwa wa Covid-19 ni “virusi vya China” – akiwa anatoa taarifa hiyo, alitoa barakoa mfukoni kwake, lakini hakuivaa.
Rais huyo ana kibarua kigumu wakati anapotafuta kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi wa urais Novemba dhidi ya mpinzani wake wa chama cha Democratic, Joe Biden, kulingana na kura za maoni.
Bwana Biden Jumanne alimshutumu Bwana Trump kwa kushindwa kukabiliana na janga la virusi vya corona. “Amewaondokea nyinyi, ametenga nchi hii,” aliyekuwa makamu rais wa Marekani alisema.
Kufuata yaliyokuwa yameandikwa tu
Donald Trump ameanza tena kutoka taarifa kuhusu virusi vya corona. Bila kuzingatia alichosema, ukweli tu wa kwamba ameanza tena kutoa taarifa juu ya corona kunaashiria mengi kuhusu athari hasi ya janga hilo ambazo zimekumba Marekani katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Maambukizi yanazidi kuongezeka, hasa kusini na magharibi, hilo pengine moja kwa moja limetokana na hatua ya utawala wake ya kusitisha kanuni za kuzuia usambaaji kabla ya malengo ya wizara ya afya kufikiwa.
Hivyo basi rais alijitahidi sana kuzungumza kulingana na taarifa aliyoandaliwa, na bila kujikanganya akakiri huenda hali ikawa mbaya zaidi kabla ya kuanza kuimarika. Baada ya kipindi kilichotangulia kudai kwamba mwanahabari aliyekuwa amevaa barakoa kuwa yuko sahihi kisiasa”, sasa ahamasisha watu kuvaa barakoa.
Kura za maoni za hivi karibuni zimeonesha kwamba anaendelea kupoteza uungwaji mkono na umma kama rais kuhusu jinsi anavyoshughulikia janga la virusi vya corona wakati anatafuta kuchaguliwa tena.
Ikulu ya Marekani ina imani ya kumwezesha rais kuwa tena chaguo la raia wa Marekani na kufanikisha kurejesha imani ya uongozi wake kwa raia.
Hata hivyo kwa changamoto ya rais sasa hivi kupata ufumbuzi, ni pale tu maambukizi yatakapoanza kupungua, wagonjwa kupungua hospitalini, raia wa Marekani watakaporejea makazini, shule zitakapofunguliwa, na maisha kurejea kidogo kama ilivyokuwa kawaida. Na siku hiyo bado inaonekana kuwa mbali, huku uchaguzi ukikaribia.
Bwana Trump alikuwa peke yake bila wataalamu wa afya ambao awali pia nao walikuwa wakitoa taarifa kwa vyombo vya habari. Kauli zake zilikuwa fupi na zenye kuonesha muelekeo, akikwepa kujibizana na wanahabari waliouliza maswali kidogo.
Aliendelea: “Tunawataka Wamarekani wavae barakoa, wazingatie kutokaribiana na kutekeleza usafi wa juu – nawa kimono yako kila unapopata fursa ya kufanya hivyo.
“Tunaomba vijana wa Marekani kuepuka maeneo ya baa yaliyosongamana na mikusanyiko mingine ya ndani. Kuwa salama na mwenye akili.”
Bwana Trump mwenyewe amekuwa havai barakoa mbele ya vyombo vya habari, akidai kwamba baadhi ya watu wanavaa tu barakoa ili kutoa taarifa za kisiasa dhidi yake. Hivi karibuni, vyombo vya habari vilimpiga picha akiwa amevaa barakoa kwa mara ya kwanza wakati alipokuwa anatembelea hospitali ya jeshi.
Alipoulizwa Jumanne kuhusu kubadilika kwake hadi kuanza kuunga mkono uvaaji wa barakoa, rais alisema kwamba hata wataalamu wa afya wamebadili mawazo yao.
Machi, Dkt. Anthony Fauci, mmoja wa viongozi wa jopo la rais la kukabiliana na virusi vya corona, na mpasuaji maarufu Marekani Jerome Adams walisema hakuna sababu ya raia wa Marekani kuvaa barakoa.
Lakini tangu Aprili, Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Marekani (CDC) kimetoa wito kwa raia wa Marekani kuvaa barakoa wanapokuwa maeneo ya umma.
Dkt. Fauci sasa anasema kwamba mamlaka ya Marekani inastahili kutumia nguvu kuhakikisha raia wanavaa barakoa, ingawa Bwana Trump amekataa wito wa Ikulu ya Marekani kutoa agizo la kuvaa barakoa kwa lazima.
Wakati wa mkutano huo, aliendeleza dai la kwamba siku moja ugonjwa huo utatokomea.
Pia alitoa dai la uongo kwamba Marekani ina “idadi ndogo ya vifo vinavyotokana na virusi vya corona, kuliko kwengine kokote duniani”.
Kulingana na chuo kikuu cha Johns Hopkins, idadi ya vifo Marekani inaorodheshwa ya 10 kati ya nchi 20 zilizoathirika vibaya na janga la virusi vya corona duniani.
Marekani imerekodi karibia maambukizi milioni 3.9 ya ugonjwa wa Covid-19 ikiwa na vifo zaidi ya 141,000 miongoni mwa idadi kubwa duniani.
Bwana Trump pia aliulizwa na mwanahabari kuhusu Ghislaine Maxwell, mwenye ushawishi katika mitandao ya kijamii ambaye alihukumiwa mwezi huu na mamlaka ya Marekani kwa makosa ya ulanguzi wa watoto kingono kwa ajili ya aliyekuwa mchumba wake, aliyehukumiwa kwa makosa ya uhalifu wa kingono marehemu Jeffrey Epstein.
Rais alisema: “Sijafuatilia sana kesi hiyo. Ukweli ni kwamba namtakia kila la kheri. Nimekutana naye mara kadhaa, hasa tangu nilipokuwa ninaishi eneo la ufuo la Palm [Florida], na nafikiri pia wao waliishi ufuoni Palm.”
“Sijui hali ya mwanamfalme Andrew,” Bwana Trump aliongeza, akizungumzia Andrew wa familia ya Kifalme Uingereza, ambaye amekanusha madai kuwa alishiriki mapenzi na wasichana wadogo anayesema alisafirishwa na Epstein.