Na: GLADNESS MFULU
Imeelezwa kuwa Takribani watu milioni 600 duniani kila mwaka wanaugua maradhi yatokanayo na chakula ambacho si salama, ambapo zaidi watu laki 4 hufariki dunia kutokana na maradhi ya tumbo, asilimia 40 wakiwa ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wajawazito pamoja na wazee.
Mhadhiri na Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Teknolojia ya Chakula, Lishe na Sayansi ya Mlaji kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Dkt. Rashid Suleman, amesema hayo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani na kuongeza kuwa chakula ambacho kimeharibika na ambacho si salama kinaweza kusababisha madhara makubwa kwa mlaji.
Akizungumza na SUAMEDIA ikiwa ni siku chache kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Usalama wa Chakula Duniani ambayo huadhimishwa tarehe 7 June kila mwaka.
Akizungumzia kuhusu siku hiyo na malengo yake Dkt. Suleman amesema lengo kuu ni kuelimisha dunia kuhusu uchafuzi wa chakula na maji, ambayo ndio huleta madhara makubwa kwa binadamu kutokana na kuwa ni mahitaji muhimu kwa maisha ya binadamu.
“kuna malengo matano ambayo yamewekwa na shirika la chakula Duniani pamoja na shirika la Afya Duniani ili kuadhimisha siku ya chakula duniani la kwanza ni to ensure it safety yaani hakikisha ni salama na hii ni kwa ngazi ya serikali, serikali ihakikishe yakuwa chakula ambacho kinapatikana ni salama alafu kina virutubisho kwa wananchi wote hiyo ni level ya serikali, lakini kuna level ya mzalishaji ambayo wanasema grow it safe zalisha ambacho ni salama, kwahiyo kama ni mzalishaji uzalishe chakula ambacho ni salama lakini kuna level ya mfanyabiashara tunasema keep it safe hakikisha unakiweka salama, lakini kwenye level ya mtumiaji make sure that its safe unaeenda kununua chakula uhakikishe kina ubora”
Aidha ameeleza baadhi ya vyanzo vya uchafuzi wa chakula na kutaja chanzo kikubwa kuwa ni Sumu Kuvu au Fangasi ambayo ni tatizo kubwa kwa sasa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, katika nchi za Kitropiki na sambamba na Kemikali, Baolojia pamoja na Virusi.
Kauli Mbiu ya mwaka huu ya Maadhimisho ya siku ya Usalama wa Chakula Duniani ni ‘Chakula salama leo kwa Afya njema kesho’.