Na Farida Mkongwe
Morogoro
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kipo kwenye mchakato wa kuandaa sera ya kudhibiti udhalilishaji wa kingono ili kutatua changamoto ya udhalilishaji huo katika maeneo ya chuo.
Rasi wa Ndaki ya Kilimo Prof. Bernard Chove akisoma hotuba ya ufunguzi ( Picha zote na Vedasto George)
Akifungua warsha ya kujadili rasimu ya sera hiyo kwa niaba ya Makamu wa Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda, Rasi wa Ndaki ya Kilimo Prof. Bernard Chove amesema sera hiyo ni muhimu hususani katika kipindi hiki ambacho Serikali imeanza kuchukua hatua dhidi ya udhalilishaji huo wa kingono katika maeneo mbalimbali ya nchi hususani vyuoni.
Prof. Chove amewataka wadau wanaoshiriki kwenye warsha hiyo kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha sera hiyo ili ilete manufaa kwa chuo na umma kwa ujumla.
Maoni hayo yatasaidia sana kuboresha sera hii na kusaidia kuimarisha mifumo yetu ya kudhibiti udhalilishaji wa kingono miongoni mwa wafanyakazi, wanafunzi na wadau wengine wa Chuo”,“ amesema Prof. Chove.
Mkuu wa Mradi mdogo wa namna ya kufanya mazingira ya kazi kuwa salama kutokana na udhalilishaji wa kingono Dkt. Fatihiya Massawe akitoa neno katika warsha hiyo
Kwa upande wake Mkuu wa Mradi mdogo wa namna ya kufanya mazingira ya kazi kuwa salama kutokana na udhalilishaji wa kingono Mhadhiri Mwandamizi kutoka Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia Dkt. Fatihiya Massawe amesema sera hiyo itakapokamilika itawasaidia watu kupata uelewa wa namna ya kujikinga na udhalilishaji wa kingono.
“Matarajio yetu sera hii itakapokamilika suala la unyanyasanyaji na udhalilishaji wa kingono halitakuwepo tena kwa sababu wanafunzi, wafanyakazi na wadau wengine hapa chuoni watapata elimu ya kutosha ya namna bora ya kuviripoti vitendo vya aina hiyo na hivyo kuweza kufanyiwa kazi kwa mujibu wa matakwa ya sera na sheria za utumishi wa umma”, amesema Prof. Fatihiya.
Rasi wa Ndaki ya Kilimo Prof. Bernard Chove aliyekaa katikati amevaa suti, Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia Dkt. Samwel Kabote aliyekaa kulia na DkT. Fatihiya wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano huo