Na.Vedasto George
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema kuazishwa kwa mifumo mbalimbali ya TEHAMA kutasaidia kusambaza huduma za ugani kwa wakulima ili kupambana na changamoto ya upungufu wa maafisa ugani na uwepo wa tija katika kilimo.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya katika ya shamba akikagua moja ya mashamba ya mfano SUA, kulia mbele ni Makamu wa Mkuu SUA Prof Raphael Chibunda
Kusaya ameyasema hayo wakati akizungumza na menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA lengo likikiwa ni kijitambulisha na kujadili namna ya kuboresha kilimo hapa nchini.
Aidha Kusaya amebainisha kuwa tafiti nzuri zinazoibuliwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA zinazohusu kilimo ni lazima ziwafikie wakulima ili kuleta tija katika sekta hii muhimu.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo amesema Serikali imejipanga na inaendelea kutoa elimu ya kutosha kwa wakulima ili kuondoa dhana ya muda mrefu ya kuwa kilimo ni chaguo la mwisho la watu kujiajiri.
Wakati huohuo Bw. Kusanya amekutana na vijana wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini wanaoendelea na mafunzo kwa vitendo kuhusu kilimo biashara katika kituo atamizi cha vijana ambapo amewata vijana wengine kujitokeza na kupata mafunzo kuhusu kilimo na kuweza kujiajiri wenyewe.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya akiangalia mimea katika moja ya atamizi SUA
Akieleza manufaa ya kituo hicho Bi. Hefsiba Olloo kutoka mkoa wa Kilimanjaro amesema ameweza kuzalisha nyanya kwenye kitalu nyumba na kuvuna kilo 1,318 za nyanya zilizompatia shilingi milioni 4 ndani ya kipindi cha miezi minne.
“Kwa muda mfupi tangu nimejiunga na kambi atamizi hapa SUA mwezi septemba 2019 tayari nimeona manufaa makubwa ya kuwa na uhakika wa kipato kupitia kilimo cha nyanya” amesema Hefsiba
Naye msimamizi wa kituo hicho cha atamizi kwa vijana Zebedayo Sanga ambaye ni muhitimu wa shahada ya kilimo cha matunda na mbogamboga katika Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA amesema yeye kama msimamizi ameendelea kuwahamasisha vijana kijifunza kilimo.