Prof. Jumanne Abdallah akitoa ufafanuzi katika warsha ya kujadili kozi mpya SUA
Na Gerald Lwomile, Dar es Salaam
Mkuu wa Idara ya Uchumi Misitu na Mazingira Prof. Jumanne Abdallah amesema kozi mpya ya Misitu Biashara, Ujasiriamali na Masoko inayotarajiwa kuanzishwa SUA inaweza kufundishwa katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Diploma, Shahada ya Kwanza na hata Shahada za Juu kama ambavyo wadau mbalimbali wameshauri
Prof. Abdallah amesema hayo katika warsha ya siku moja ya kujadili namna bora ya kuendesha kozi hiyo na iwekwe katika ngazi ipi warsha iliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni
Amesema wao kama Idara chini ya Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii iliyopendekeza kozi hiyo ni muhimu wakafuata maoni ili kulisaidia Taifa, wahitimu na wakulima wa zao la miti nchini
Katika hatua nyingine wakulima wa miti nchini wametakiwa kujua taratibu za kupanda miti hasa kwa kuzingatia upandaji wa awamu ili kuwa uvunaji endelevu ambao utawasaidia pia kupata kipato kila wakati na hivyo kuwaletea matokea mazuri katika kilimo Biashara cha miti
Hayo yamesemwa na Mhadhiri Mwandamizi kutoka Ndaki ya Misitu, Wanyapori na Utalii Prof. Felister Mombo wakati akitoa ufafanuzi wa kozi mpya ambayo inatarajiwa kuanzishwa SUA itakayoandaa wahitimu katika kozi ya Misitu Biashara, Ujasiriamali na Masoko
Prof. Mombo amesema wakati mwingine inashangaza kuona mtu ana shamba la ukubwa wa ekari kadhaa na anaamua kulipanda miti lote na kusubiri hadi miaka kadhaa kabla ya kuvuna wakati angeweza kupanda shamba hilo kwa awamu huku akiacha eneo jingine litumike kwa uzalishaji wa mazao ya muda mfupi
Amesema haya ni baadhi ya mambo ambayo mkulima akifundishwa yatamsaidia kuhakikisha anakuwa na kipato kwa muda wote.
Warsha hiyo ya siku moja ambayo imefanyika jiji Dar es Salaam ilikuwa na lengo la kutaka kupata maoni ya wadau kuhusu kozi hiyo mpya.