Na Gerald Lwomile
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA leo Mei 20, 2020 kimezindua mafunzo kwa wakufunzi Chuoni hapo ya namna ya kufundisha kwa njia ya mtandao yaani “Online Training” ili kuhakikisha kinawafikia wanafunzi na wadau wengine wengi zaidi ambao wanahitaji kupata mafunzo mbalimbali kutoka SUA.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kaimu Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo upande wa Taaluma Prof. Maulid Mwatawala amesema hiyo ni hatua kubwa ambayo SUA imepiga na kuwataka wakufunzi wote wanaopata mafunzo hayo kuhakikisha wanajenga timu imara itakayohakikisha inasaidia katika kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao kwa ufasaha.
Kaimu Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo upande wa Taaluma Prof. Maulid Mwatawala akizindua mafunzo kwa njia ya mtandao (Picha zote na Gerald Lwomile)
Prof. Mwatawala ameongeza kuwa wakufunzi hao kutoka Ndaki zote, Shule kuu na Maktaba ya Taifa ya Kilimo iliyopo SUA wanatakiwa kuhakikisha kunakuwa na hali ya undelevu wa utoaji mafunzo kwa njia ya mtandao ili kuhakikisha wanafikia malengo yaliyokusudiwa.
Akizungumzia agizo la Serikali la kufungwa kwa vyuo vyote nchini kufuatia ugonjwa wa Corona COVID-19, Prof. Mwatawala amesema Chuo kimeona kuna haja ya kuhakikisha kinaendelea kufanya kazi yake ya kufundisha kwa kutumia njia mbadala kama mafunzo kwa njia mtandao na hiyo ni sababu mojawapo iliyosukuma kuwepo kwa mafunzo hayo.
Awali akimkaribisha Kaimu Naibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitalaamu Prof. Erson Karimuribo amesema kazi ya kuandaa kanuni na taratibu za uendeshaji wa mafunzo hayo zilianza mara tu baada ya Kurugenzi hiyo kwa kushirikiana na Kurugenzi ya TEHEMA chuoni hapo kuwasilisha andiko katika kikao cha Bodi ya Chuo kilichofanyika hivi karibuni.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitalaamu Prof. Erson Karimuribo akitoa maelezo ya mchakato wa mafunzo hayo
Aidha, mkurugenzi amewashukuru wadau wote ikiwa ni pamoja na Menejimenti ya Chuo, Kurugenzi ya TEHEMA na wote walioshiriki katika kuhakikisha utoaji mafunzo kwa njia ya mtandao unafanikiwa. Mara baada ya wakufunzi hao kupata mafunzo hayo wataanza kutoa msaada na mafunzo kwa waalimu watakaokuwa wakitoa elimu kwa njia ya mtandao.
Mafunzo kama haya yanatarajiwa pia kutolewa kwa wanafunzi wanaotarajia kusoma kwa njia ya mtandao.
Wakufunzi wakipewa mafunzo ya namna ya kufundisha kwa njia ya mtandao