Na Farida Mkongwe
Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigella amewataka watanzania hususan wakazi wa mkoa wa Morogoro kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye wiki ya Kumbukizi ya Edward Sokoine pamoja na kumlaki na kumsikiliza Makamu wa Rais Mh. Dkt. Philip Mpango ambaye atakuwa mgeni Rasmi katika kufunga wiki hiyo.
Shigella ametoa wito huo Mei 25 mwaka huu wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Kumbukizi hiyo inayofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA ambapo siku ya Alhamisi Mei 27 Makamu wa Rais atafunga Rasmi wiki hiyo iliyoanza Mei 24 Mwaka huu na kwamba maandalizi yote yameshakamilika.
“Nitoe wito kwa wakazi wa mkoa wa Morogoro tujitokeze kumlaki Makamu wetu wa Rais kwani hii ni mara yake ya kwanza kuja mkoani kwetu tangu achaguliwe kuitumikia nafasi hii, niwaombe sana wana Morogoro tuoneshe ukarimu wetu katika kumpokea na kumsikiliza kiongozi wetu”, alisema Shigella.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa wa Morogoro amekipongeza chuo cha SUA kwa kuweka utaratibu mzuri wa kuthamini na kuwaenzi viongozi waliotenda mambo mazuri kwa taifa na kuwataka wananchi wakajionee Teknolojia mbalimbali zinazooneshwa na Chuo hicho katika wiki hiyo ya Kumbukizi.
Kwa upande wake Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda amemshukuru Makamu wa Rais Mh. Philip Mpango kukubali kuwa Mgeni Rasmi katika ufungaji wa wiki hiyo ya Kumbukizi ya Sokoine na kutoa wito kwa Wafanyakazi na Wanafunzi wa SUA pamoja na watanzania kwa ujumla kushiriki katika tukio hilo muhimu.
Wiki ya Kumbukizi ya Hayati Sokoine imebeba Mada isemayo Teknolojia za Kilimo, Kuzalisha kwa Tija na Ushindani katika Soko Nchini Tanzania Kuelekea Nchi ya Uchumi wa Kati wa Juu.