Na:Tatyana Celestine
Katika kuhakikisha tafiti za kisayansi zinazidi kuwa bora na kuleta tija nchini Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimewakutanisha waalimu, watafiti wachanga na wanafunzi wa Shahada ya Uzamivu SUA ili kuwajengea uwezo katika kuandaa na kufikisha tafiti zao kwa jamii

Akizungumza katika ufunguzi wa warsha ya siku tano iliyoandaliwa na Kurugenzi ya Uzamili,Utafiti,Uhaulishaji Teknolojia na Ushauri wa kitaalamu (DPRCT), Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Amandus Muhairwa ambaye amemuwakilisha Makamu wa Mkuu wa Chuo Hicho Prof. Raphael Chibunda, amewataka washiriki kutambua kuwa ni muhimu kwa mtafiti kuhakikisha anatoa mrejesho wa utafiti aliofanya
Prof. Muhairwa amesema SUA imeendelea kufanya vizuri katika kuandaa tafiti bora Afrika na duniani, pia imekuwa ya kwanza upande wa Vyuo Vikuu Tanzania kupitia matokeo ya ‘Webometric’ Julai 2020 na kuwa SUA imekuwa ikitenga fedha ili kuongeza tija na kuendelea kufanya vizuri.
Aidha Prof. Muhairwa ameongeza kuwa chuo kimekuwa kikitoa machapisho ya kisayansi kwa lengo kuipatia jamii uelewa hivyo kupitia warsha hiyo makosa madogo yataepukwa katika maandalizi ya machapisho yajayo kwani wataweza kuwa mahiri kuandika, kupitia kwa umakini na kuwasilisha maandiko ya kisayansi kwa kuzingatia kanuni itakayojibu maswali yote katika tafiti kwa jamii.
Kwa upande wake Mratibu wa Utafiti na Machapisho SUA kupitia Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu (DPRCT), Prof. Japhet Kashaigili amesema kuwa tafiti za chuo cha SUA zimekuwa zikifanya vizuri na kuleta tija hivyo amewataka watafiti kuhakikisha wanazitafsiri na kutumia lugha rahisi ili ziweze kumfikia mlengwa
Alipotakiwa kuungumizia kuhusu tafiti ambazo hucheleweshwa au kutowafikia walengwa Prof. Kashaigili amesema kuwa kwa wale wenye tatizo hilo sababu hutegemeana na hoja yenyewe, mchango katika maendeleo, imechapishwa kwa njia gani na ina mvuto kiasi gani kwa kushindwa kuonesha vigezo hivyo kupelekea kuishia kuwa za kielimu pekee ama kubaki kabatini.