Na: Farida Mkongwe
Jumla ya wahitimu 149 wametunukiwa Shahada, Stashahada na Astashahada za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA katika Mahafali ya 37 ya Katikati ya Mwaka ya Chuo hicho ambayo yamefanyika leo Mei 28.
Akizungumza katika mahafali hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Michezo vya SUA, Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda amesema kati ya wahitimu hao wanaume ni 92 sawa na asilimia 61.8 na wanawake ni asilimia 38.2
Wanafunzi waliotunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa ni 15 kati yao wanaume wakiwa 15 na wanawake 10 huku wanafunzi waliotunukiwa Shahada za Uzamili wakiwa 51, wanaume 23 na wanawake 28
Aidha Prof. Chibunda amewataka wahitimu kuyatumia mafanikio waliyoyapata kuwa chachu ya kuzalisha mali na kuliendeleza taifa katika sekta mbalimbali za kiuchumi
“Ni matumaini yetu kuwa mafanikio haya yatakuwa chachu ya kuzalisha mali na kutoa huduma bora, mkawe mabalozi wazuri wa chuo chetu lakini pia mkatumie elimu mliyoipata kuwa wabunifu, wajasiriamali na ikiwezekana mkazalishe ajira kwa wengine”, amesema Prof. Chibunda.
Awali akizungumza katika Mahafali hayo Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Mh. Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande amesema Baraza hilo limeisimamia ipasavyo Menejimenti ya SUA katika kutekeleza majukumu yake ya kiutafiti pamoja na kutekeleza Mpango Mkakati wa chuo hicho
“Katika Kipindi hiki tangu kufanyika kwa Mahafali iliyopita, tumeweza kutekelza Mpango Mkakati wa Chuo, kuidhinisha bajeti ya Chuo, kusimamia miradi, kufanya teuzi za viongozi mbalimbali……..”, amesema Jaji Mstaafu Mh. Chande.
Hii ni Mahafali ya 37 ya Chuo cha SUA tangu kuanzishwa kwake lakini ni ya kwanza kufanyika katikati ya mwaka tangu Baraza la Chuo liliporidhia kufanyika mahafali mara 2 kwa mwaka ili kutoa nafasi kwa wanafunzi wanaohitimu masomo yao mwanzoni mwa mwaka kutunukiwa Shahada zao mapema badala ya kusubiri Mahafali za mwisho wa mwaka.
Video