Na: Catherine Mangula Ogessa
Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Isdori Mpango , amewataka wadau wote mtambuka wa Sekta ya Kilimo kutambua kuwa wanasafari kubwa wakishirikiana na Serikali kuona ni kwa kiasi gani wanawajibu wa kulifaulu somo la Hayati Edwardi Moringe Sokoine katika kuinua uzalishaji, tija na masoko ya mazao ya Kilimo.
Mh. Dkt Mpango ametoa wito huo wakati akifunga Maadhimisho ya 17 ya Wiki ya Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA mjini Morogoro
Dkt. Mpango amesema kuwa Hayati Sokoine miongoni mwa mambo aliyokuwa akiyawekea mkazo ni pamoja na kujitosheleza kwa chakula, kuwekeza katika kilimo na ufugaji, na utafiti kama msingi wa maamuzi ya kutunga au kuhuisha sera na kubadilisha maisha ya wananchi vijijini kuwa bora zaidi.
“Maadhimisho haya kwanza yanatoa fursa kwa wataalami wa kilimo, wakulima, watunga sera, wanasiasa na wadau kutoka makundi mbalimbali kutafakari mawazo na uongozi wa Hayati Edward Moringe Sokoine hususan mwelekeo wa maendeleo ya kilimo nchini….
“kwa maoni yangu lengo moja kuu la tafakuri hiyo linapaswa kuibua mikakati na kubuni mbinu mpya za kufikia maoni ya Hayati Sokoine yanafanikisha mapinduzi ya Kilimo ili kuinua maisha ya wananchi vijijini katika mazingira ya sasa na zama hizi za teknolojia ya habari na Mawasiliano.” Makamu wa Rais Dkt. Mpango
Makamu wa Rais ameongeza kuwa pamoja na jitihada za Hayati Sokoine katika Sekta ya Kilimo, wadau wote wa kilimo wanatakiwa kutambua kuwa pamoja na umuhimu wa Kilimo katika uchumi, tija ya kilimo bado hairidhishi kutokana na namna ambavyo wakulima wamekuwa wakizalisha.
Aidha Dkt. Mpango ameyaagiza makampuni yote yanayoagiza mbegu nje ya nchi kuhakikisha yanazalisha hapa nchini na pia Wizara ya Kilimo ihakikishe inafuatilia suala hilo.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekipongeza Chuo cha SUA kwa kuwa na kauli mbiu ya mwaka huu ambayo amesema kuwa ina akisi mipango na mikakati ya serikali ya awamu ya sita inayojielekeza kukuza uzalishaji katika kilimo kama msingi wa maendeleo ya viwanda kama ilivyoainishwa katika mkakati wa kuendeleza Sekta ya Kilimo na Mpango wa tatu wa maendeleo wa Taifa .
Mbali na pongezi hizo Makamu wa Rais pia ametoa agizo kwa Chuo Kikuu cha SUA kuhakikisha kinaandika kitabu cha Historia ya Hayati Edward Moringe Sokoine, na pia kumtaka waziri wa Elimu kuhakikisha anaratibu suala la kuwepo kwa kumbukumbu za Sokoine katika shule ya Sekondari iliyopo Wami Dakawa.
Awali akitoa neno kwa mgeni rasmi Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo SUA Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba amesema SUA inahitaji msaada mkubwa ili kuweza kufanikisha malengo makuu likiwemo suala la utafiti ambao utawasidia watu walioko vijijini kuondokana umaskini
“ Nchi imefika hatua kubwa mapaka tumeingia katika uchumi wa kati lakini bado tunamatatizo makubwa hasa katika eneo la umaskini na wengi wao wale walio vijijini wakulima , wafugaji, na wavuvi,………… kwa chuo kikuu cha SUA
“kazi wanazozifanya kwa bidii pamoja na utafiti wanahitaji msaada mkubwa ili utafiti huo uwafikie Wakulima, Wafugaji na Wavuvi.” Jaji Mstaafu Warioba.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amemtaja Hayati Sokoine pamoja na mengine lakini alipigania maendeleo ya ustawi wa Taifa hasa katika sekata ya Kilimo na Mifugo, lakini pia alitilia mkazo nchi kujitosheleza katika chakula pamoja na kusimamia utekelezaji mkubwa wa Kilimo na Mifugo na kutoa msisitizo wa wakulima na wafugaji kuweza kulima kisasa na tija.
Aidha Prof. Ndalichako amefafanua kuwa “ Mheshimiwa makamu wa Rais umejionea vijana wetu wanapata mafunzo ya hali ya juu kabisa na wanaweza hata kushiriki katika kuzalisha Teknolojia ambazo zinaweza kumsaidia mkulima wamefika hatua ya kuweza kutengeneza matrekta hii ni hatua kubwa sana tunaomba Serikali iendelee kutuunga mkono ili vijana walioonesha ubunifu tuweze kuwaendelea.”
Kwa upande wake makamu wa Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema kuwa SUA imekuwa ikimuenzi kwa kuwa na wiki ya Kumbukizi ya Sokoine kutokana na umuhimu wake katika chuo kwani kwa jinsi alivyosimamia wakati wa Muswada bungeni ili chuo hiki kiwerze kuwa chuo kikuu na baada ya kumalizika kwa shughuli hizo za bungeni wakati akirudi Dar es Salaam ndipo alipopata ajali.
Prof. Chibunda amefafanua kuwa SUA inatambua jinsi alivyokuwa shupavu, mzalendo wa kweli mwadilifu na katika kuyaenzi hayo yote katika mwaka huu wamekuwa na maonesho ya Teknolojia na ubunifu katika kuzalisha mazao, ufugaji na uvuvi, Kongamano la Kisayansi, Huduma za Hospitali yaani upimaji na kuchangia Damu Salama lakini pia kumekuwa na michezo.
Kwa upande wa msemaji wa Familia ya Hayati Sokoine ameipongeza SUA kwa namna ambavyo kimekuwa kikimuenzi Sokoine, laini pia kauli mbiu ya mwaka huu inaakisi mambo ambayo Sokoine aliyafanya, lakini pia kikatoa ombi kwa SUA kuhakikisha wanandika kitabu cha historia ya Sokoine.
Maadhimisho ya Kumbukizi ya hayati Sokoine yamehushuriwa na viongozi mbalimbali akiwepo Waziri mkuu mstaafu awamu ya nne Mizengo Pinda, mkuu wa mkoa wa Morogoro Martini Shigela, viongozi wa Dini pamoja Siasa.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu inayosema “Teknolojia za Kilimo, Tija na Ushindani katika Soko: Tanzania kuelekea Nchi ya Uchumi wa kati wa juu.”