NA GLADNESS MPHURU
Imeelezwa kuwa Panya waitwao Search and rescue Rat wanaopata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wanaweza kusaidia kwenye utafutaji na uokoaji wa binadamu, wakati wa majanga hususan katika vita.
Hayo yameelezwa Mei 26 na Mtafiti Msaidizi wa Kituo cha Utafiti wa Ugunduzi wa Teknolojia Mpya juu ya Viumbe Hai Waharibifu kilichopo chini ya Apoppo Said Mshana, katika Maonesho ya Wiki
ya Kumbukizi ya Edward Moringe Sokoine inayofanyika SUA mjini Morogoro.
Amesema changamoto kubwa inayowakabili waokoaji duniani na ambayo haijapata ufumbuzi hadi sasa ni utafutaji wa binadamu katika majanga hususan yaliyosababishwa na vita au majengo kubomoka, ambao ukifanywa na panya hao kutoka SUA unawezekana kutokana na udogo wa miili yao na hivyo kuweza
kuingia popote bila vikwazo.
Mshana amesema panya ni moja kati ya viumbe wanaoweza kufundishika kiurahisi, hivyo ameeleza wanavyowapatia mafunzo panya hao ambayo ni pamoja na kuwaweka katika mazingira ya kuwa Rafiki wa binadamu pampja na kunusa harufu ya binadamu ili waweze kufanya uokoaji kwa wahanga wote.
Amesema katika zoezi hilo la uokoaji kwa kutumia panya huwafunga mgongoni kifaa maalum kilichounganishwa na kompyuta, ambacho kina kamera lengo likiwa ni kuonesha kilichopo mbele yake wakati wa kuwatafuta wahanga, kinasa sauti, kitunza kumbukumbu na kifaa cha kuonesha alipo kwa ajili ya kutoa taarifa za mahali alipo muhanga ili zoezi la uokoaji liweze kufanyika.
Aidha amesema teknolojia hizo zinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uokoaji kwenye nchi zenye vita akitolea mfano Israel na Palestina, kutokana na kuwa binadamu wengi hupotea katika vita hivyo.