Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimefanikiwa kuongeza idadi ya Programu mbalimbali za masomo kufikia 116 ukilinganisha na programu tatu wakati Chuo hicho kinaanzishwa mwaka 1984.
Mafanikio hayo yamewekwa bayana na Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda wakati akielezea baadhi ya mafanikio SUA tangu kuanzishwa kwake kwenye ufunguzi wa Wiki ya Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine inayofanyika katika Kampasi ya Edward Moringe iliyopo SUA mkoani Morogoro.
Prof. Chibunda amesema katika kutekeleza majukumu yake makuu ya Kufundisha, Utafiti na Ugani, SUA pia imefanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi na kufikia 14,581 kwa mwaka wa masomo 2020/2021 ukilinganisha na wanafunzi 400 tu wakati Chuo hicho kinaanzishwa.
Mafanikio mengine ni Kupanua shughuli za Chuo sehemu mbalimbali nchini ili kusogeza huduma karibu na wananchi katika mikoa ya Morogoro, Arusha, Katavi, Ruvuma, Tanga, Iringa na Njombe, ambapo katika Nyanja ya utafiti SUA ilishika nafasi ya kwanza nchini kwa kupata nukuu (citations) 89,752 kwenye Google scholar.
“Pia tumeendelea kupanda kwa nafasi ya ubora wa Chuo katika Vyuo Vikuu bora duniani ambapo kwa matokeo yaliyotolewa na Taasisi ya Webometric ya mwezi Januari 2021 SUA ilishika nafasi ya 53 kwa ubora katika Vyuo Vikuu bora 200 katika Bara la Afrika na kushika nafasi ya pili nchini nyuma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilichoshika nafasi ya kwanza kitaifa na nafasi ya 41 katika Bara la Afrika”, amesema Prof. Chibunda.”
Ameongeza kuwa SUA uchapisha wastani wa machapisho ya kitaalamu 500 kwenye majarida mbalimbali yanayotambulika kitaifa na kimataifa, kupata wastani wa miradi ya utafiti 120 yenye wastani wa thamani ya sh. bilioni 25 kwa mwaka pamoja na Chuo kuweza kupata hataza 13 (patents) katika baadhi ya maeneo ya tafiti, ugunduzi wa mbegu mbalimbali za mazao, vyakula na lishe, uzalishaji wa miche ya matunda kwa njia ya chupa, chanjo na visumbufu vya mazao na mifugo;
“Katika kutimiza majukumu yetu SUA imeweza kushindana na taasisi nyingine za Elimu ya Juu Duniani na kuweza kushinda miradi mikubwa ya utafiti, baadhi ya miradi hiyo ni Kituo cha Taifa cha Uratibu wa Hewa ya Ukaa (NCMC) chenye mradi wenye thamani ya Krona za Norway Milioni 37 na Kituo cha Utafiti wa Magonjwa Ambukizi cha Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (SACIDS) chenye miradi yenye thamani ya dola za Kimarekani Milioni 25”, amesema Prof. Chibunda.
Aidha Prof. Chibunda amesema SUA kwa kushirikiana na Wakfu wa PASS kimeanzisha Kituo Atamizi cha Vijana kwa ajili ya kuwafundisha vijana Kilimo Biashara, kuanzisha mashamba darasa ya mfano kwa ajili ya kufundishia wanafunzi, wakulima na wadau wengine mafunzo kwa vitendo pamoja na kufanikisha Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ikiwemo maabara, madarasa, karakana za uhandisi, maktaba, barabara, mabweni, nyumba na ofisi za wafanyakazi kwa uwezeshaji wa serikali, mapato ya ndani na washirika wa maendeleo.