Na: Catherine Mangula Ogessa
Serikali imeombwa kuendelea kufadhili kwa kuwezesha Vyuo Vikuu ili vifanye tafiti ambazo zina tija kwa nchi na ambazo zinalenga kutatua matatizo ya taifa kwani kupitia tafiti ndiko kunako patikana maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Utafiti na Machapisho kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Japhet Kashaigili wakati akieleza mambo ambayo wameweza kujadili katika Mdahalo wa Kisayansi ambao umekutanisha watafiti mbalimbali hapa nchini pamoja na wengine kutoka nje ya nchi.
Prof. Kashaigili amesema kuwa Serikali hainabudi kuendelea kuwezesha katika tafiti kwani tafiti nyingi ambazo zimekuwa zikifanywa zinatokana na miradi toka nje ambayo kwa namna moja ama nyingine zinaweza zisisaidie kutatua matatizo yaliyopo nchini.
“Kuna umuhimu mkubwa sana kuwekeza katika tafiti na ubunifu, kwani kwa siku mbili watafiti tumeweza kujadili ni namna gani sayansi pamoja na teknolojia zinavyoweza kuchangia katika kuinua au kuleta maendeleo ya nchi kutoka katika uchumi wa kati wa chini kuelekea uchumi wa kati wa juu.” Prof. Kashaigili.
Akielezea kuhusu mdahalo huo wa Kisayansi Prof. Kashaigili amebainisha kwamba katika mkutano huo mengi yameweza kujadiliwa kutokana na Teknolojia zilizo wasilishwa namna bora ya kulima na kufuga, namna ya kukabiliana na magonjwa lakini piaTeknolojia ya umwagiliaji kwa kutumia maji kidogo lakini kwa tija.
Mdahalo huo wa siku mbili kumekuwa na mawasilisho toka Uingereza, Zambia, Nigeria pamoja na Malaysia lakini kwa hapa Tanzania mbali na SUA kumekuwa na mawasilisho toka Chuo Kikuu cha Dodoma, pamoja na Taasisi za TAFIRI, TALIRI.
Aidha amesema kwa sasa wanajukumu la kuhakikisha wanayachakata mawasilisho hayo na baadae waweze kuyaandika katika lugha rahisi ambayo itamsaidia mkulima pia lugha itakayosaidia katika kufanya maamuzi.
Mdahalo huo wa Sayansi umekuwa ni Mdahalo ni miongoni mwa shughuli ambazo zimefanyika katika Maadhimisho ya 17 katika Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine kama moja kuenzi mchango wake katika Sekta ya Kilimo.