Na: Tatyana Celestine
Watafiti nchini wametakiwa kutafsiri matokeo ya tafiti zao kulingana na jamii iliyokusudiwa ili kuleta tija na ufanisi kwani kutofanya hivyo kunaweza kupelekea matokeo ya utafiti kutoeleweka.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Ndaki ya Sayansi ya Jamii na Insia SUA Prof. Samwel Kabote ambaye amemuwakilisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) upande wa Taaluma Profesa Maulid Mwatawala wakati akifunga warsha ya kuwajengea uwezo katika kuandaa na kufikisha tafiti kwa jamii.
Prof. Kabote amesema kuwa mafunzo hayo ni ya muhimu hivyo wanatakiwa kuyafanyia kazi ipasavyo na hasa mambo ambayo wamejifunza ili chuo kiendelee kushika nafasi ya kwanza kwa tafiti bora nchini na hata duniani.
Aidha Prof. Kabote amesema washiriki wamepata mafunzo yatakayo wawezeshe kuwa mahiri katika kuandika, kupitia kwa umakini na kuwasilisha maandiko ya kisayansi kwa kuzingatia kanuni itakayojibu maswali yote katika tafiti kwa jamii kwani chuo kimekuwa kikitoa machapisho ya kisayansi kwa lengo kuipatia jamii uelewa wa kina na kuahidi kuwa chuo kitandelea kutoa mafunzo kama hayo kwa watafiti wachanga.
Kwa upande wake Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu kitengo cha Ugani na Maendeleo ya Jamii SUA Bw. Juma Almasi amesema kuwa mafunzo waliyopata yameweza kuwasaidia kutambua umuhimu wa kutafsiri matokeo ya tafiti ambapo husaidia kumfanya mlengwa kuelewa vema na kufanyia kazi matokeo ya utafiti husika.
“Tuchukulie umefanya utafiti juu ya madhara yanayoshambulia Maharagwe na wewe ukashindwa kutafsiri vizuri madhara yake unayoyaona kwenye utafiti wako ili wakulima waweze kuyatumia na kulima mazao katika itakiwavyo ili kuwasaidia kupata mazao ya kutosha…..ipo wazi ukishindwa kutafsiri vizuri ni kama vile utafiti wako haukuwa na maana yeyote” amesema Almasi
Aidha Mwanafunzi huyo amesema kuwa SUA imekuwa chachu katika uandaji wa tafiti bora nchini na imekuwa ikiwasaidia wananchi wa chini ambapo wanaendelea na shughuli za kilimo na mifungo.
Katika hatua nyingine Bw. Almas ameiomba Menejimenti ya Chuo, Taasisi zingine pamoja na Serikali kuongeza bajeti kwa ajili ya watafiti ili kuwezesha watafiti ambayo itasaidia kutoa matokeo bora,yenye tija na uhakika jamii na nchi kwa ujumla.
Warsha hiyo ya siku tano iliyoandaliwa na Kurugenzi ya Uzamili,Utafiti,Uhaulishaji Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu (DPRCT) kwa lengo la kuwajengea uwezo katika kuandaa na kufikisha tafiti zao yameshirikisha zaidi ya wahitimu 20 ambapo pia wametunukiwa vyeti