Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda amewashauri Wanataaluma na Watanzania wengine kuona umuhimu wa kuweka mawazo yao katika vitabu ambayo yatasaidia kubadili fikra na mitazamo ili kuchochea maendeleo ya Tanzania.
Wito huo umetolewa wakati wa kupokea Vitabu kumi vyenye thamani ya shilingi laki nne vilivyotolewa na Mwanafunzi wa SUA ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Cliford Tandali ambapo kitabu kilichoandikwa na Bwana Derek Murusuri kinachoitwa Making Africa world’s largets Economy yaani “Kuifanya afrika kuwa yenye uchumi mkubwa Duniani”.
Prof. Chibunda alisema kuna watu wenye mawazo mazuri ambayo yanaweza kuisaidia Tanzania na Afrika lakini wamebaki nayo vichwani mwao na wengine wanaandika na kuishia njiani hivyo kuifanya jamii na taifa kushindwa kunufaika na mawazo yao mazuri.
“Nakupongeza sana Bwana Derek kwa kufanikiwa kuandika na kukamilisha kitabu hiki ambacho kinakwenda sasa kwa jamii kukisoma ili kuleta maendeleo ya taifa letu na Afrika kwa ujumla,na mawazo yako yataishi hata utakapoondoka duniani’’ Alisema Prof. Chibunda.
Kwa upande wake Dkt. Cliford Tandali amabye ndiye aliyetoa msaada wa vitabu hivyo kwaajili ya Maktaba ya Taifa ya Kilimo ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA alisema kuwa wanafunzi wa somo la Taaluma za Maendeleo na Ndaki ya Sayansi za Jamii na Insia vitabu hivyo vitawafaa kutokana na mawazo mazuri yaliyowekwa humo.
Dkt. Tandali alibainisha kuwa kitabu hicho baada yayeye kukisoma kinaonyesha kwa uwazi na undani namna ambavyo nchi mbalimbali duniani zimefanya na kupiga hatua kimaendeleo hasa katika matumizi ya Sayansi na Teknoloji na sasa wako mbali hata wale ambao tulipata uhuru pamoja nao.
“Mabara mengine yamesonga mbele kwa kuzingatia Sayansi Teknolojia na Ubunifu hivyo sisi kama watanzania tuna kila sababu ya kuikumbatia Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ili tuweze kupiga hatua kwa haraka kama ambavyo wenzetu wamefanya’’Alisema Dkt. Tandali.
Aliongeza kwa kusema kuwa SUA ndio mahali ambapo masomo ya sayansi yanafundishwa na teknolojia zinazalishwa hivyo ametoa wito kwa Serikali kuona sababu ya kutenga fungu maalumu ili matokeo ya tafiti hizo ziweze kusambazwa na kuisaidia jamii ya watanzania hasa zile za kilimo,mifugo na uvuvi.
Nae Mwandishi wa kitabu hicho kilichozinduliwa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda amemshukuru Katibu Tawala wa Mstaafu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Cliford Tandali kwa kutimiza maagizo ya Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda aliyoitoa wakati akizindua kitabu hicho ya kutaka kitabu hicho kisambazwe vyuo vikuu ili vijana wengi wakisome.
Akielezea malengo ya kuandika kitabu hicho alisema ni kuwaamsha,kuwahamasisha vijana ili kuwa chachu kwani wanaweza kulifanya Bara la Afrika kuweza kushindana kiuchumi na nchi za mabara mengine kwa kubadili mitazamo,kuchapa kazi na kutumia maliasili zilizopo.
‘’Hili linawezekana kabisa kwa kuvunja kizuizi cha utamaduni kuwa hatuwezi hasa kwa vijana wetu walio kwenye vyuo vikuu na taasisi zingine katika kutumia teknolojia na ubunifu kama njia muhimu ya kuleta mageuzi katika eneo hilo nyeti na muhimu katika karne ya sasa inayotegemea sana sayansi na teknolojia’’ Alisisitiza Derek Murusuri.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maktaba ya Taifa ya Kilimo ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Mugyabuso Lwehabura akipokea vitabu hivyo kutoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo ameahidi kuvitunza na kuwapatia wanafunzi na watumiaji wa Maktaba hiyo kuvisoma na uhitaji ukiwa mkubwa wataongeza idadi yake ili mawazo ya mwandishi wa kitabu yatimie.
Fuatilia katika video hapa chini