Na: Gerald Lwomile
Wanafunzi waliojiunga na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wametakiwa kutumia maboresho ya miundombinu yanayofanywa chuoni kuhakikisha wanafikia matarajio yao ya kusoma na kuweza kujiajiri ama kuajiriwa.
Akizungumza katika siku ya kilele cha kuyajua mazingira ya chuo maarufu kama “Orientation Week” Naibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Peter Gillah ambaye alimwakilisha Makamu wa Mkuu wa Chuo SUA Prof. Raphael Chibunda, ameeleza hivi sasa Chuo kinaendelea na mchakato wa kurekebisha na kuongeza miundombinu ya elimu ili mwanafunzi anapotoka chuoani awe ameiva
Amesema chuo kinaendelea na ujenzi wa Maabara mtambuka kubwa ya kisasa lakini pia kinafanyia marekekebisho maabara nyingine na kimeanzisha mashamba darasa ambayo kama mwanafunzi ataamua na kujikita katika kuhakikisha anafikia malengo basi miundonbinu hiyo ipo
Akizungumzia jinsi wanafunzi hao walivyopata nafasi ya kujiunga na chuo hicho amesema wote walioingia wamekidhi vigezo na kuwa watembee kifua mbele kwani wanasoma katika chuo ambacho kwa ubora ni chuo cha pili nchini Tanzania kati ya vyuo vyote vikuu vilivyopo nchini na cha 74 katika zaidi ya vyuo elfu tatu vilivyoko barani Afrika
Naye Naibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA upande wa Utawala na Fedha Prof. Yasinta Muzanila amewataka wanafunzi kuhakikisha kila wanapotoka chuoni hapo wanakuwa na ruhusa maalumu kwa kufuata taratibu zilizowekwa na chuo kwa lengo la kulinda usalama wa mwanafunzi
Aidha Prof. Muzanila amewataka wanafunzi kuhakikisha wanafuata sheria zilizowekwa ikiwa ni pamoja na kuacha kupika chakula kwenye mabweni, kutochezea vifaa vya umeme, kuacha kutumia lugha za matusi na za kudharirisha katika jinsi zote
Akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi Mashauri wa Wanafunzi SUA Bw. Pule Motshabi amesema ofisi ya Mshauri wa Wanafunzi iko wazi wakati wote na itatoa ushirikiano kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanasoma katika mazingira rafiki