Na Gerald Lwomile, Kongwa
Jamii ya wafugaji na wakulima katika wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma iko katika hatari kubwa ya kukosa malisho ya wanyama na maeneo ya kilimo kufuatia kuwepo kwa gugu hatari maarufu kama Gugu Kongwa au Mahata kuendelea kueneo kwa wingi katika maeneo mbalimbali wilayani humo
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Dkt. Suleiman Serera akiongea na waandishi wa habari wakati wa mrejesho wa utafiti kuhusu namna ya kudhibiti Gugu Kongwa
Hayo yamesemwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Dkt. Suleiman Serera wakati wa mrejesho wa utafiti kuhusu namna ya kudhibiti Gugu Kongwa uliotolewa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wilayani humo hivi karibuni
Dkt. Serera amesema endapo gugu hilo litaendelea kuenea katika maeneo mengi wilayani humo linaweza kusababisha kuwepo kwa upungufu mkubwa ya malisho kwani wakazi wengi katika wilaya ya Kongwa ni wafugaji ambao hata hivyo wamekuwa na maeneo machache ya malisho jambo ambalo mara nyingine husababisha ugomvi baina ya wakulima na wafugaji
Amesema pamoja na kuwepo kwa Gugu Kongwa lakini pia ni vyema watafiti hao wakaangalia namna ya kuliona kama fursa kwa kufanya tafiti zaidi namna gani linaweza kutumika kwani magugu kama hayo mara nyingine ni vigumu kuyaondoa kabisa katika maeneo ambayo tayari yameenea kwa wingi
“Kwa hiyo tunataka hii mimea waingalie maana wao waliangalia eneo moja tu kuwa ni tatizo wakilenga kupata malisho zaidi lakini sisi tunataka waiangalie je hata kama malisho tunakosa lakini mimea hii inaweza kufanya kitu gani kingine?” amesema Dkt. Serera
Akitoa matokeo ya awali baada ya utafiti wa miaka miwili ulioanza mwaka 2019 Mkuu wa Mradi huo Dkt. Ismail Suleiman amesema kwa sasa Gugu Mahata limeendelea kumea katika maeneo mengi mkoani Dodoma na kuwa hatua za kitafiti bado zinaendelea ili kujua ni namna gani Rafiki ya kudhibiti gugu hilo
“Aidha mikoa yenye mazingira yanayopendelewa sana yaani ‘highly suitable’ na gugu hili ni Dodoma, Singida na Manyara lakini pia mikoa mingine inayopendelewa kwa wastani yaani ‘suitable’ ni mikoa ya Arusha, Lindi, Tanga, Kilimanjaro, Mtwara, Morogoro na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini” amesema Dkt. Suleiman
Dk Suleiman ameongeza kuwa maeneo yanayopata wastani mdogo wa mvua kwa mwaka kuanzia milimita 500 hadi milimita 800 hupendelewa zaidi na gugu hili aidha maeneo yanayopata mvua nyingi zaidi katika mwezi wa kwanza Januari hupendelewa zaidi na gugu hili.
Mkuu wa Mradi huo Dkt. Ismail Suleiman akionyesha mbagu Melia zinazoweza kupandwa ili kuotesha mti huo
Amesema Gugu hilo linapendelea zaidi kumea katika maeneo ya machunga na kilimo hasa yaliyopumzishwa na linakuwa vizuri katika mchanganyiko wa udongo wa kichanga, mfinyanzi na tifutivu
Naye Mtafiti Mwanafunzi ambae amefanya utafiti wa namna ya kuangamiza gugu hilo Bw. Notkery Mwalongo amesema majaribio mengi ya kudhibiti gugu hilo yamefanyika ikiwa ni pamoja na kutumia miti na mazoa adui wa gugu hilo kama Nyonyo, Melia au Mwarobaini Jike na Tumbaku ambapo mti wa Melia umeonesha kufanya vizuri katika kudhibiti gugu hilo
Mti wa Meli ambao unaweza kutengenezwa kemikali zinazoua gugu Kongwa
Mwalongo amesema pamoja na kuwepo kwa matokeo hayo yanayonesha mti aina ya Melia kufanya vizuri katika kukabiliana na gugu hilo bado changamoto ni kubwa katika kuhakikisha mti huo unazalishwa kwa wingi ili kukabiliana na gugu hilo
“Kwa mfano mti huo aina ya Melia unaweza kuua hili gugu kwa kiasi gani, lakini pia bado tunachangamoto ya kwamba lazima tuone namna ya kuzalisha kwa wingi ili kuweza kuvuna na kutengeneza kemikali kwa ajili ya kunyunyizia ili kuweza kuliua hili gugu” amesema Mwalongo
Naye Prof. Antony Sangeda pamoja wa watafiti katika mradi huo amesema sababu ya kufanya utafiti wa gugu hilo wilayani Kongwa ni baada ya kuonekana asili ya gugu hilo wilayani hapo japo kuna uwezekano kuwa lililetwa kutokana na eneo hilo kuwa na historia ya kukaliwa na wapigania uhuru wa nchi zilizoko Kusini mwa Afrika
Aidha Mwenyekiti wa Kijiji cha Sejeri Kata ya Sejeri wilayani Kongwe Bw. Amos Mizengo amesema awali wenyeji wa maeneo hayo waliona gugu hilo kama sehemu ya maua na wengine walithubutu hadi kulipanda katika maeneo yao jambo ambalo lilipelekea kuenea kwa kasi kwa gugu hilo
Amesema hivi sasa gugu hilo limezunguka katika vijiji zaidi ya 10 vinavyoizunguka Ranchi ya Taifa ya NARCO na kusababisha uhaba mkubwa wa malisho kwani gugu hilo linapoota hutawala katika eneo husika na kutoruhusu nyasi au malisho mengine ya mifugo kuota katika eneo hilo.
Gugu Kongwa likiwa limekauka (Picha zote na Gerald Lwomile)