Viongozi Wakuu wa Vyuo Vikuu nchini wameipongeza Serikali ya Awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya maamuzi makubwa ya kujenga Reli ya kasi SGR pamoja na Mkandarasi wa Reli hiyo kwa kazi nzuri wanayaifanya usiku na mchana ili kukamilisha reli hiyo kwa wakati.
Akiongea Mara baada ya kutembelea Andaki Refu zaidi kati ya mahandaki yanayojengwa Mwenyekiti wa Kamati ya Makamu wakuu wa vyuo vyote vya Umma na Binafsi ambaye ni Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda amesema ujenzi wa Reli hiyo utakuwa chachu katika kuleta maendeleo Tanzania.
Amesema lengo la ziara hiyo kama viongozi wa wasimamizi wa Vyuo vikuu nchini ambavyo vinazalisha wataalamu katika fani mbalimbali kwa maendeleo ya Taifa ni kujionea maendeleo ya mradi huo wa kipekee na wa aiana yake Afrika mashariki.
Prof. Chibunda amesema kupitia ziara hiyo sasa wanaweza kuona ni kwa namna gani wataweza kuzalisha wataalamu ambao watasaidia kuendeleza na kuendesha Reli hiyo pale itakapokamilika lakini pia wamefarijika kuona vijana wengi wa kitanzania ambao ni wahitimu wa vyuo wamepata ajira pia wanavyoshiriki kujifunza ili kampuni hiyo ya ujenzi itakapoondoka waweze kuiendesha.
“ Sisi leo tunashukuru tumejionea wenyewe kwa macho yetu na hapa tupo Viongozi Wakuu wa Vyuo 38 na wengine wameshindwa kutokana na majukumu makubwa ya kiakazi hivyo tumeridhika na kufarijika na maendeleo ya mradi huu ambao unagharimiwa na fedha za kodi za Watanzania na sio wafadhili “ Alisema Prof. Chibunda.
Nae Prof. Yohana Msanjila ambaye ni Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha St. Johns cha Dodoma amesema haya ni maendeleo makubwa ambayo Tanzania imepiga katika kufanikisha ujenzi huu wa Reli ambao utasaidia sana katika kuongeza kasi ya maendeleo.
“ Mradi huu ukikamilika nakuhakikishia Tanzania utapiga hatua kubwa za za haraka za maendeleo kutoka hapa tulipo sasa” Alisisitiza Prof. Msanjila.
Prof. Faustine Karrani ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM amesema kazi hii iliyofanywa na Serikali ya awamu ya tano ni kazi nzuri na kubwa na yenye faida kubwa kiuchumi na kijamii hasa katika kuimarisha usafirishaji na uchukuzi nchini katika historia ya nchi yetu.
“ Tumefurahishwa kwa hatua hii kazi hii ni kubwa na zuri na tunaamini utakapokamilika utaketa mageuzi makubwa sana kwa nchi yetu ya Tanzania” Prof. Karrani.
Kwa upande wake Rasi wa Chuo Kishiriki cha Mkwawa Iringa Prof. Esther Dungumaro amesema kujenga mradi huu ni uthubutu wa hali ya juu kwa Serikali ya awamu ya tano kwenye kujenga Miradi mikubwa ya aina hii ambao umetumia fedha nyingi.
“Nampongeza sana Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutekeleza mradi huu kwa fedha za Tanzania na ninaamini kwa uthubutu huu tunaiona Tanzania ya kipekee sana kimaendeleo” Alisema Prof. Ester.
Nae Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Prof. Charles Dominick Kihampa amewapongeza viongozi hao wa Vyuo Nchini kwa kuamua kutembelea Mradi huo na kuona wahitimu kutoka kwenye Vyuo vyao wanavyoshiriki katika Ujenzi na kuona ni kwa namna gani wanavyoweza kuboresha Elimu wanayoitoa ili kuendana na mahitaji ya soko.
“ Zipo sehemu nyingi ambazo watanzania wataweza kunufaika kupitia Mradi huu wa Reli lakini nimefarijika sana kama msimamizi wa ubora wa elimu vyuoni kuona viongozi hawa wa Vyuo wametembelea Mradi huu maana sasa wataweza kuona aina za programu wanazoweza kuanzisha ili utakapokamilika tuwe na watanzania ambao wataweza kutekeleza miradi mingine kama hii mikubwa ambayo nchi yetu itahitaji kuijenga” Alisisitiza Prof. Kihampa.
Viongozi hao wa Vyuo Vikuu nchini wapo kwenye ziara ya siku mbili kutembelea Reli hiyo ya SGR kutoka Dodoma hadi Dar es salaam ili kujionea maajabu ya Ujenzi wa Reli yenyewe, Mahandaki na madaraja makubwa.