Na: Calvin E. Gwabara
Masele Jilala Mkazi wa Kijiji cha Idukilo Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga amebuni trekta la kulimia na gari ya kutembelea kwa kutumia mashine ya kusaga na hivyo kurahisisha shughuli za kilimo na usafiri kwa wanakijiji wenzake.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Idukilo, Kishapu amesema kuwa ubunifu huo ulitokana na changamoto kubwa waliyokuwa nayo wanakijiji wa Idukilo wa kuchelewa kulima mashamba na hivyo kupitwa na msimu kutokana na kutokuwepo kwa huduma za matrekta kijijini hapo.
Mbunifu huyo Ndugu Jilala amesema alilima shamba na kupata fedha ambazo zilimuwezesha kununua vifaa kama vile injini ya mashine ya kusaga, “Gear box” Chakavu na vifaa vingine vinavyohitajikka na kisha kuanza kuunganisha hadi kukamilisha.
Amebainisha kuwa ubunifu huo aliuanza mwaka 1990 kwa kutengeneza na kufumua kila alipoona haikai anavyotaka hadi kukamilika vizuri mwaka 2015 ambapo alijaribu kwa kulima mashamba yake na kuanza kuwalimia wanakijiji wengine.
Jilala amesema trekta hiyo ina uwezo wa kulima ekari 5 hadi 8 kwa siku baada ya kufunga “gear box” kubwa wakati “gear box” ya awali ndogo ilikuwa na uwezo mdogo na kubainisha kuwa kwa sasa anatafuta njia ya kufunga majembe mawili badala ya moja alilokuwa natumia awali.
Mbunifu huyo amesema pia amefaniswa kutengeneza gari la kutembelea baada ya serikali kumsaidia fedha za kununua matairi ili kuendeleza ubunifu wake na sasa gari hilo analitumia yeye na familia yake pamoja na wanakijiji wengine.
Katika video