Na Gerald Lwomile,Dar es Salaam
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii inakusudia kuanzisha kozi ya Misitu Biashara, Ujasiliamali na Masoko ikiwa ni mkakati wa makusudi wa kutoa wahitimu katika fani ya misitu ambao wataenda kuinua mnyororo wa thamani wa misitu nchini.
Naibu wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Utawala na Fedha Prof. Yasinta Muzanila aliyeshika pochi katikati akiwa katika picha na wadau wa warsha
Hayo yamesemwa Novemba 7, 2019 jijini Dar es Salaam na Naibu wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Utawala na Fedha Prof. Yasinta Muzanila ambaye amemwakilisha Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda
Prof. Muzanila amesema kama kozi hiyo itafanikiwa kuanzishwa basi inaweza kuongeza wigo wa wanafunzi kushiriki kikamilifu katika kuongeza pato la taifa kupitia sekta ya misitu nchini.
Amesema kozi hii ni ya kipekee kwani itaweza kumfanya mhitimu kuwa na fani katika misitu, uchumi, ujasirimali, masoko na biashara na hivyo kuondoa changamoto ya ukosefu wa ajira kwani mtu ataweza kujiajiri mwenyewe na wakati mwingine kusaidia wakulima wa miti kuendesha zao hilo kibiashara.
“Kwa upande mwingine kuna changamoto mpya katika elimu ya misitu, kwa mfano wahitimu wengi wana matarajio ya kuajiriwa katika maeneo ya mjini mara baada ya kuhitimu kozi zao huku utaalamu wao ukihitajika zaidi katika maeneo ya vijijini kitu kinachopelekea kushindwa kutatua mahitaji ya jamii” amesema Prof. Muzanila
Naibu wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Utawala na Fedha Prof. Yasinta Muzanila wa kwanza kilia akifuatilia kwa makini mawasilisho katika warsha hiyo
Akizungumza kuhusu kuanzishwa kwa kozi hiyo mpya, Rais wa Shirikisho la Viwanda vya Misitu Tanzania Bw. Ben Mfungo Sulus amesema Serikali ya sasa inalenga kuinua uchumi kwa njia ya viwanda hivyo kozi hii imekuja wakati muafaka na itainua sekta ya misitu kwani ni eneo mojawapo linalotoa malighafi za viwanda.
Akizungumzia umuhimu wa kuanzisha kozi hiyo Mhadhiri Mwandamizi katika Ndaki ya Misitu, Wanyapori na Utalii Prof. Felister Mombo amesema upo umuhimu wa kuhakikisha kunatengenezwa muunganiko wa masuala ya misitu, uchumi na biashara ili kutatua changamoto mbalimbali za kibiashara kwenye secta ya misitu.
Katika warsha hiyo ya siku moja wahadhiri waandamizi Prof. Yonika Ngaga na Prof J.M. Abdallah Mkuu wa Idara ya Uchumi Misitu na Mazingira walionyesha namna kozi hii itakavyo somwa na masomo yapi na itafundishwaje, warsha hii imeshirikisha wadau kutoka Serikalini, Sekta binafsi na Wataalam Mbalimbali.