Na Gladness Mafuru
Imeelezwa kuwa kupitia machapisho yanayo tolewa na kitengo cha Maktaba ya Mkulima kilichopo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kinaweza kuleta tija kwa mkulima na Taifa kwa ujumla katika kuelekea Tanzania ya Viwanda.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Idara Maktaba ya Mkulima SUA Dr. Wulystan Mtega wakati akizungumza na SUAMEDIA ofisini kwake Mei 4,2021.
Dr. Mtega amesema kuwa Maktaba ya Mkulima imekuwa fursa kwa wakulima nchini kutokana na kutatua hangamoto ya wakulima kupata ugumu wa kukutana na maafisa Ugani, hivyo mkulima anaweza kutembelea Kitengo hicho au kutumia machapisho yanayopatikana katika Ghala la Maktaba ya Mkulima bila gharama yeyote.
Ameongeza kuwa lengo hasa la kuanzishwa kwa ghala hilo ni kumfikia mkulima moja kwa moja ambapo hadi hivi sasa limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kupitia Maonesho ya Nanenane, kutembelea maeneo baadhi yaliyopo kandokando ya Mji wa Morogoro pamoja na
mkakati wa kuanzisha Runinga ya Mkulima “Library”.
Aidha amesema kwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali kutoka SUA wanaendelea kutengeneza machapisho ya kilimo yanayoendelea kuwasaidia wakulima kutatua changamoto ya Magonjwa ya Mifugo na Mimea ili kuleta tija.
Dr. Mtega ametoa wito kwa wakulima haswa wa mkoani Morogoro kuitumia Maktaba hiyo ya Taifa inayopatikana chuoni SUA ili kuwa mabalozi wazuri kwa watanzania wengine kwaajili ya kukuza uzalishaji wa malighafi katika kuelekea Uchumi wa Viwanda.