NA GLADNESS MPHURU
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimekabidhi Damu Salama kiasi cha unit 123 kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Damu ambayo ilipatikana katika Maonesho ya Wiki ya Kumbukizi ya Edward Moringe Sokoine, kwa lengo la kuimarisha uhusiano baina ya Hospitali hiyo na Hospital za SUA.
Makabidhiano hayo yamefanyika June 2, 2021 na aliyekuwa Mwenyekiti wa Maadhimisho ya Kumbukizi ya Sokoine Prof. Samweli Kabote kwa niaba ya
Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda, yakishuhudiwa na Dkt. Erhard Kapilima kwa niaba ya Daktari Kiongozi wa Hospitali za SUA.
Prof. Kabote amesema katika kumuenzi Hayati Edward Sokoine Chuo hicho hufanya shughuli mbalimbali ikiwemo huduma za Afya, na kwa mwaka huu huduma mojawapo ilikuwa ni pamoja na kuchangia damu kwa hiari, na kuongeza kuwa bila ya afya bora maendeleo hayawezi kupatikana.
Ameongeza kuwa ukusanyaji huo wa damu ulifanywa na makundi mbalimbali ya watu, ambapo kundi kubwa lilikuwa ni wanafunzi wa Chuo hicho, Wafanyakazi wa SUA na kundi la mwisho ni la Wananchi wa Manispaa ya Morogoro kwa ujumla.
“Kwa mwaka huu huduma mojawapo ya kijamii ilikuwa ni kuchangia damu kwa hiari na kulikuwa na shughuli nyingine ambazo zilikuwa zinafanyika ikiwemo upimaji wa magonjwa mbalimbali ili kuweza kuhakikisha kwamba jamii yetu ina nguvu kazi ambayo inaweza ikafanya kazi kwa ufanisi na ukaleta maendeleo kwa jamii, kwahiyo leo tumekuja tu hapa kwa ajili ya kukabidhi kiasi cha damu ambacho kimepatikana kutokana na hizo shughuli za kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine”, amesema Prof. Kabote
Kwa upande wake Mmganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro Dkt. Kusirye Boniface Ukio, ametoa shukrani nyingi kwa uongozi wa SUA, kwa kuona umuhimu wa kuchangia Damu salama kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi hususan kina mama wanaojifungua, watoto, pamoja na waathirika wa ajali.
Pia ametoa tathmini za kimkoa kuwa asilimia 70 ya vifo vya kina mama vinatokana na kupoteza damu nyingi baada ya kujifungua, na asilimia 20 vinatokana na kifafa cha mimba na kwamba damu hiyo kutoka SUA itasaidia maisha ya wananchi kwa kiasi kikubwa.
Amesema hospitali hiyo inahitaji kiasi cha damu salama zaidi ya chupa 6,000 kwa mwaka, ambazo hukusanywa kutoka halmashauri zote za mkoa huo ikitegemea idadi ya watu katika kila halmashauri.
“Jambo lililofanyika sio jambo dogo kwa zile lugha zetu za kienyeji zetu tunasema ni life serving yaani mmegusa pale panapotakiwa kuguswa kwa sababu pia ubora wa huduma zetu popote pale zinapimwa kwa huduma za uzazi na matokeo yake, mkoa huu una vituo karibu 470 kwa Hospitali za Rufaa kwa mkoa huu ni mbili kwa maana ya Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na Hospitaki ya Mtakatifu Fransisco iliyoko Ifakara lakini tunashirikiana kwa sababu mgonjwa akitoka ifakara huja huku”, alisisitiza Mganga Mkuu.