Na Gerald Lwomile
Mara
Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mkoani Mara Bibi Lydia Bupilipili amekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa kuwaruhusu na kuchangia gharama zilizowazesha wafanyakazi wa chuo hicho kufanya utalii wa ndani jambo ambalo limekuwa likisisitizwa na serikali
Mkuu wa Wilaya ya Bunda Bibi. Bupilipili akizungumza na wadau wa utalii wa ndani ambao walipata fursa ya kufika nyumbani kwake (Picha na Gerald Lwomile)
Akiongea na wafanyakazi kutoka SUA ambao wamefanya safari ya utalii wa ndani waliopita nyumbani kwake hivi karibuni Mkuu huyo wa Wilaya amesema SUA imekuwa mfano bora katika kuhamasisha utalii ambao unaingizia mapato taifa
Akizungumzia kuhusu utalii katika mkoa wa Mara Bupilipili amesema watu wengi hawajui kuwa ili kuingia Hifadhi ya Serengeti lango kuu liko wilayani hapo
“Nyinyi ni mabalozi wa wengine, maana hata geti kubwa la kuingia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti…… watu wengi hawajui kuwa geti hilo liko Bunda…. Nasi sasa tuko katika mkakati wa kuhakikisha tunaimarisha na kuboresha utalii maana kitovu cha utalii katika mkoa wa Mara na Bunda kama ilivyo karatu mkoani Arusha” amesema Bupilipili
Wadau wa utalii wa ndani kutoka SUA wakiwa katika kaburi la Baba wa Taifa kijijini Mwitongo Butiama ambapo walipata fursha ya kutoa heshima zao na kusali kwa pamoja
Akizungumzia safari yao ya utalii wa ndani Mwenyekiti wa kikundi cha utalii wa ndani kilichopo SUA Bw. Laurent Makoa amemshukuru Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda na Menejimenti ya SUA kwa kuwawezesha kushiriki utalii huo
“Sisi wafanyakazi tunafanya kazi kwa muda mrefu hivyo wakati mwingine kupata muda wa kupumzika na kufanya utalii kama huu ni jambo jema na linaongeza uelewa wa mtu hivyo tunamshukuru Makamu wa Mkuu wa Chuo na Menejimenti kwa kutuwezesha” amesema Makao
Wadau wa utalii wa ndani kutoka SUA wakiwa hatika picha ya pamoja katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane mkoani Mwanza (Picha na Gerald Lwomile)
Amesema SUA ni Taasisi kubwa na pia inatoa kozi ya utalii hivyo ni muhimu wafanyakazi wake bila kujali nafasi walizonazo wabapata nafasi za kufanya utalii kwani kwa kufanya hivyo wanachangia pato la Taifa
Jumla ya wafanyakazi 23 kutoka kikundi hicho cha utalii wa ndani wamefanya utalii katika Makazi ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na hifadhi ya Taifa ya Saanane iliyoko kisiwani Jijini Mwanza