Na; Josephine Mallango
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimepongezwa kwa kuwa chuo kinachotoa mchango mkubwa wa utatuzi wa ajira kwa vitendo na kilichofanikiwa kuwabadilisha fikra vijana wahitimu wa vyuo vikuu nchini .
Katika picha ya pamoja Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana Mh. Antony Mavunde (wa tatu kutoka kushoto), Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda (wa tatu kutoka kulia)Mkurugenzi wa SUGECCO Revocatus Kimario (wa kwanza kushoto) pamoja na Viongozi wengine.
Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana Mh. Antony Mavunde ameyasema hayo wakati akikabidhi tiketi kwa vijana 12 wahitimu wa SUA wanaokwenda nchini Marekani kupitia programu ya mafunzo kwa vitendo kwa wanachama wa SUGECCO.
Amesema uwepo wa SUA kwa miaka ya hivi karibuni unaonekana kwa vitendo hasa katika kutatua changamoto ya ajira kwa vijana na uthubutu wa chuo hicho kuwabadili vijana kifikra hali inayowafanya vijana hao kuwaza kujiajiri kupitia kilimo kutokana na mafunzo wanayopata wakiwa chuoni .
Naibu Waziri huyo amewaasa vijana wanaokwenda Marekani kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri wa chuo cha SUA na Tanzania kwa ujumla na kurudi na ujuzi wenye tija kwa Taifa.
Kwa upande wake Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda ameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuleta fedha za maendeleo chuoni pamoja na kuihakikishia serikali kuwa SUA itaendelea na program mbalimbali ambazo zitaendelea kuleta tija kwa Taifa.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Prof. Peter Gillah ametoa pongezi kwa SUGECCO kwa kuanzisha program hiyo ya mafunzo ya kuwapeleka vijana katika nchi mbalimbali na kuwaasa vijana wanaosafiri kuhakikisha wanarudi na maarifa tofauti yatakayoleta chachu kwa vijana na mabadiliko nchini katika sekta ya kilimo
Kwa upande wake Mkurugenzi wa SUGECCO Revocatus Kimario amesema wameandaa program nyingine kwa ajili ya vijana hao ili pindi watakaporudi waweze kuutumia ujuzi watakaoupata kuwanufaisha vijana wenzao na taifa kwa ujumla.
Vijana hao 12 wanaungana na vijana wengine 75 na kufikia vijana 87 waliokwenda kwa nyakati fofauti nchini Marekani kwa ajili ya mafunzo ya vitendo na kwa sasa wanakwenda katika maeneo ya mashamba ya kuku, mashamba ya nguruwe na mashamba ya mboga mboga .
Zaidi katika picha