Na Gerald Lwomile
Morogoro
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amesema tatizo la uadilifu katika sehemu za kazi ni kubwa jambo linaloweza kuleta madhara makubwa kiuchumi na kijamii
Prof. Chibunda akizungumza na wafanyakazi wapya wa SUA
Prof. Chibunda amesema hayo Julai 22, 2021 wakati akifungua Mafunzo ya Maadili kwa wafanyakazi wapya wa SUA, ambayo yamelenga kuwapa uelewa wafanyakazi hao juu ya umuhimu wa kuzingatia maadili kazini
Amesema kuwa kuna baadhi ya watumishi wamekuwa wakishiriki katika ubadhirifu wa mali za umma, rushwa na hata wizi wa vifaa mbalimbali vya kutolea huduma katika maeneo ya kazi na kukwamisha utendaji wa kazi katika maeneo mbalimbali
“Unakuta Mhudumu ambaye anatembea na mafaili ya ofisi anatoa siri za ofisi ikiwa ni pamoja na kutoa nakala na kuanza kusambaza nje na kwenye mitandao ya kijamii” amesema Prof. Chibunda
Akizungumzia kuhusu tahadhari ya ugonjwa wa COVID 19, Prof. Chibunda amesema tayari Serikali imetoa taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa huo nchini na ni muhimu kwa wafanyakazi kuhakikisha wanachukua tahadhari ya ugonjwa huo kwa kuhakikisha wananawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, kutumia vitakasa mikono na kuvaa barakao sehemu zenye mikusanyiko ya watu
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kuthibiti Uadilifu (KKU) SUA Prof. Christopher Mahonge amewaeleza washiriki wa mafunzo hayo kuwa KKU ina jukumu la kuwa kiungo kati yake na Ndaki, Kurugenzi, Shule Kuu, Idara na Jumuiya ya Wanafunzi katika masuala ya uadilifu
Prof. Chibunda aliyevaa tai katikati akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wapya wa SUA
Amesema wameendelea kuwasiliana na wafanyakazi na wanafunzi kuhusu uadilifu na kupokea taarifa za malalamiko kuhusu ukiukwaji wa maadili yakiwemo masuala ya rushwa kutoka kwa wafanyakazi na wanafunzi chuoni hapo
Mafunzo hayo ya siku mbili kuhusu uadilifu SUA yameanza Julai 22, 2021 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 23, 2021 ambapo jumla ya wafanyakazi 330 wanatarajiwa kupata mafunzo hayo