Na: Tatyana Celestine
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Mpina (MB) amesema kuwa muda mfupi tangu Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli iingie madarakani imefanikiwa kuongeza kiwango cha ukusanyaji mapato ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi kutoka billion 21 hadi shilingi bilioni 72.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Mpina (MB) akizumza na wakati akizindua Agenda ya Kitaifa ya Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji kwa mwaka 2020/ 2025
Waziri Mpina ameyasema hayo Jumamosi tarehe 16 Novemba 2019 wakati akizindua Agenda ya Kitaifa ya Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji kwa mwaka 2020/ 2025 uliyofanyika Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo SUA Kampasi ya Solomon Mahlangu amesema kuwa kwa mwaka ujao wa fedha Sekta ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kuongeza mapato zaidi na kufikia kiasi cha shilingi bilioni 80.
Amesema licha ya ongezeko la matapato, Serikali kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kudhibiti uingizwaji holela wa zao la Mifugo na Uvuvi nchini kitendo kilichokuwa kinapelekea Wafugaji na Wavuvi wa ndani ya nchi kukosa soko na ushindani kukosekana kwani wanafuga lakini hawapati soko.
“Nataka niwambie ya kwamba hadi leo uwagizaji wa samaki kutoka nje umeshuka kwa asilimia 67 na mwaka huu tunaoenda hata asilimia 2 haijafika ya kuagiza samaki kutoka nje ya nchi, Hiyo ina maana bilioni 56 zilizokuwa zikitumika na watanzania kuagiza samaki kutoka nje zitatumika hapahapa nchini,” amesema Waziri Mpina.
Ameendelea kusema kuwa ajira zimeongezeka kutokana na ongezeko la viwanda ambalo pia limechochea uwekezaji katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi
Akizungumzia kuhusu utafiti unaofanywa hapa nchini waziri mpina amesema kuwa watafiti wengi wamefungia tafiti zao bila kuwafikishia jamii na kwa uzinduzi huo utasaidia kufukua na kusimamia kikamilifu tafiti zifanyike ili kusaidia kutatua matatizo ya wavuvi na wafugaji.
Pia ameshukuru Uongozi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuwa wenyeji wa uzinduzi huo huku akiongeza kuwa Chuo hicho ndio chimbuko kuu la Watafiti wengi wa sekta ya Mifugo na Uvuvi nchini.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Erasto Sanare amemshukuru Waziri Mpina kwa kuchagua Mkoa wa Morogoro kuwa mwenyeji wa uzinduzi huo na kuongeza kuwa hayati Mhe. Sokoine alikuwa ni mfugji hivyo kuchagua Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kufanyia uzinduzi huo ni kumuenzi kwa vitendo na kukipa heshima chuo hicho.
Amesisitiza kuwa Mkoa wa Morogoro una wafugaji wengi hivyo amefurahi kuona uzinduzi huo umefanyika mkoani hapo kwani tafiti zitasaidia kufuga kitaalam na kutatua migogoro iliyopo kati ya wafugaji na wakulima.
Kwa upande wake Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda amesema kuwa kufanyika uzinduzi huo chuoni hapo ni kutokana serikali kutambua juhudi kubwa ambazo chuo kinachofanya lakini pia elimu kwenye kufundisha na kutekeleza Agenda na mikakati ukiwemo uliozinduliwa leo na kuahadi kuwa sehemu ya utekelezaji wa agenda hiyo.
Aidha ameiomba Wizara hiyo kutosita kushirikiana na SUA pale ambapo itaona chuo hicho kinaweza kutoa ufafanuzi au msaada katika kukuza na kuinua Sekta ya Kilimo na Uvuvi nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Erasto Sanare akishukuru wakati wa ufunguzi Agenda ya Kitaifa ya Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji kwa mwaka 2020/ 2025Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda akikaribisha ugeni wakati wa wakati wa ufunguzi Agenda ya Kitaifa ya Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji kwa mwaka 2020/ 2025
Fuatilia kilichojiri kwenye tukio hilo kwa kupitia video ifuatayo kama ilivyoandaliwa na SUAMEDIA …
SOMA PIA: NDAKI YA KILIMO YASHIRIKI UZINDUZI WA AGENDA ZA UTAFITI WA MIFUGO, UVUVI NA UKUZAJI WA VIUMBE MAJI