Na: Calvin Gwabara
Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH imeliwezesha Kongano la Nguo Morogoro (KONGUMO) kushiriki maonesho mbalimbali nje na ndani ya nchi na hivyo kupanua masoko na kuongeza kipato kwa wanachama wake.
Akiongea na Waandishi wa habari kwenye maonesho ya kitaifa ya Sayansi teknolojia na Ubunifu yanayofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma Muwezeshaji wa Kongano ambaye ni Mkurugenzi wa Mama Halima African Fassion Saida Msuya amesema kuwa kupitia mafunzo na kuunganishwa pamoja kumewawezesha kukabili changamoto mbalimbali katika sekta ya nguo na hivyo kuongeza ufanisi na tija.
Akieleza faida za umoja huo Bi. Msuya amesema kuwa kupitia umoja wao wamekuwa wakishiriki maonesho mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kwa wao kupeleka wawakilishi na kazi zao na hivyo kutanua soko kutoka Tanzania pekee lakini sasa wanakwenda Kenya,Uganda Sudani Kusini na Rwanda ambapo mfano mzuri ni soko kubwa walilopata la nguo ndefu kwenda Rwanda.
Amesema kuwa Kongano hilo lilianza mwaka 2013 baada ya kuwezeshwa na COSTECH likiwa na wanachama 50 na baada ya mafunzo waliweza kuongezeka na kufikia 90 hali ambayo iliongeza ufanisi na ushirikiano katika kufanya kazi hasa zinapotokea kazi kubwa na kumaliza kwa wakati.