Katikati ya vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi ya Afrika magharibi ya Sierra Leone ,Uingereza ilijikuta kwenye mzozo wa muda mrefu wa mauaji na umwagikaji wa damu na juhudi za kurejesha amani katika miaka ya 90 nchini humo.
Katika mzozo huo ,kulikuwa na makundi kadhaa yaliyojihami,kando na kundi kuu la waasi la RUF likiongozwa na Foday Sanko .
Miongoni mwa makundi hayo lilikuwepo kundi hatari la wapiganaji kwa jina West side boys ambalo lilikuwa limejitengea ngome yake katika eneo la msituni na kutekeleza kila aina ya uhalifu .
Mnamo tarehe 25 Agosti mwaka wa 2000 kundi la West Side Boys liliwashika mateka wanajeshi 11 wa Uingereza pamoja na mwanajsehi mmoja wa Sierra Leone katika milima ya Occra kilomita 80 kutoka mji mkuu Freetown .
Wanajeshi watano waliachiliwa siku chache baadaye na kundi hilo likaendelea kuwashikilia wanajeshi wengine sita hatua iliyoharakisha kuanzishwa kwa oparesheni ya kipekee na hatari ili kuwaokoa
Kundi la la West Side boys , lilikuwa sehemu ya wapiganaji wa kijeshi waliokuwa wameitawala Sierra Leone kuanzia Mei 1997 hadi Februari 1998.
Walakini, wanachama wengi walikuwa wahalifu wa kawaida walioachiliwa kutoka gerezani wakati waasi walipofanya uvamizi mjini Freetown mnamo Januari 1999.
Kikundi hicho kiligawanyika kutoka kwa waasi wa Revolutionary United Front mwaka mmoja baadaye , kilitangaza utii kwa serikali lakini baada ya mapigano ya mara kwa mara na wanajeshi wa serikali sasa kilichukuliwa kama kundi la waasi .
Oparesheni ya kuwaokoa
Operesheni kubwa ambayo vikosi vya Uingereza viliwaokoa mateka saba walioshikiliwa na West Side Boys ilikuwa ngumu, hatari, na ilipangwa vizuri.
Hadi wanajeshi 150 na helikopta tano zilishiriki katika shambulio hilo la sehemu mbili, mapema alfajiri juu ya maficho ya msitu wa Sierra Leone.
Wakati wa kuitekeleza operesheni hiyo ulikuwa muhimu: Kulikuwa na mwangaza wa kutosha kwa helikopta hizo kuona ni wapi wanaenda, lakini hawangeweza kuonekana kwa urahisi
Kasi pia ilikuwa muhimu. Mateka walikuwa wakilindwa na wanaume na wanawake wapatao 50, ambao walikuwa tayari kuanza kufyatua risasi mara moja wanapoona helikopta
Helikopta tatu kubwa za Chinook ziliwachukua askari 110 kutoka Kikosi mashuhuri cha Parachute katika maeneo mawili ya kutua, wakati helikopta mbili ndogo za Lynx zikitoa ulinzi wa kufyatua risasi ili kuwapa kinga
Ndani ya dakika 20, mateka walikuwa kwenye helikopta, wakirudishwa maeneo salama baada ya mahangaiko ya kuzuiliwa kwa siku 16
Mashambulizi ya pande mbili
Shida kubwa zaidi iliyowakabili wapangaji wa kijeshi wa oparesheni hiyo ilikuwa kwamba West Side Boys walikuwa na kambi mbili, zilizotengwa na kilima cha umbali wa mita 300.
Nafasi moja, kusini, iliweza kutoa fursa ya shambulizi la kujikinga ili kufunika upande mwingine, kaskazini, ambapo mateka walikuwa wakishikiliwa.
Nafasi zote mbili zililazimika kushambuliwa wakati mmoja. Kambi ya kaskazini, makao makuu ya West Side Boys , ilizidiwa haraka.
Lakini upande wa kusini ulichukua muda mrefu kulemewa . Mapigano makali yaliendelea hadi saa moja na nusu, na wanajeshi wa Uingereza hata walilazimika kutumia roketi ndogo za kulipuka .
Kikundi cha west side boy kilipoteza watu 25 na karibu wapiganaji wao 18 walikamatwa, pamoja na kamanda wao.
Askari mmoja wa Uingereza aliuawa katika shambulio hilo, na mwingine alijeruhiwa vibaya. Wengine kumi na moja zaidi walipokea kile kinachoelezewa kama majeraha madogo
Matukio kabla ya Oparesheni
- 25 Agosti 2000: Wanajeshi 11 wa Uingereza watekwa nyara pamoja na mwenzao mmoja wa Sierra Leone
- 30 Agosti 2000: Wapiganaji wawaachilia wanajeshi 5 wa Uingereza
- 31 Agosti 2000: Watekaji nyara watoa matakwa ya kisiasa
- 6 Septemba 2000: mipango ya oparesheni ya kijeshi yakamilishwa
- 10 Septemba 2000: Mateka waliosalia waachiliwa
‘Operesheni kubwa’
Jeshi, Jeshi la Wanamaji na RAF zote zilitumika kushinda kundi la wapiganaji hao ambao walifikiriwa kuwa na idadi ya watu 200, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Kumekuwa na dhana isiyothibitishwa kuwa askari kikosi maalum cha SAS pia walitumiwa kutoa habari na kushiriki katika shambulio hilo.
Mchambuzi wa ulinzi Kanali Andrew Duncan alisema aliamini vikosi maalum vingekuwa “muhimu”, kuokoa mateka wakati wanajeshi wengine walitumika kuwachanganya wapiganaji wa West side boys
Wapiganaji wa kundi hilo hawakuwa na nidhamu na mara nyingi walikuwa wakinywa pombe na kutumia dawa za kulevya, lakini pia walikuwa wapiganaji wenye vifaa na waliojitolea vitani
Kundi la West Side Boys lilifanikiwa kurudi nyuma baada ya shambulio la kwanza na kisha kuwafyatulia risasi waokoaji kutoka pembeni mwa msitu.
operesheni hiyo iliendelea hadi alasiri wakati vikosi vya Uingereza vilipoamua kuondoka na kupndoa vifaa vya kivita katika msitu huo
Uzoefu wa kupigana msituni
Wapiganaji wa kundi la West Side boys walikuwa na uzoefu wa vita vya msitu, na walikuwa wakijua sana eneo hilo.Walakini, askari wa Kikosi cha Parachute ambao waliunda sehemu kubwa ya kikosi cha uokoaji pia walikuwa na uzoefu wa mapigano ya msitu.
Walihudumu nchini Sierra Leone kwa wiki tatu mapema mwaka huo kabla ya kuifanya operesheni hiyo kali
Matukio muhimu kabla ya kutekwa kwa wanajeshi wa uingereza
1999 Januari – Waasi wanaomuunga mkono kiongozi wa Revolutionary United Front Foday Sankoh wateka sehemu za Freetown kutoka Ecomog. Baada ya wiki kadhaa za mapigano makali wanafukuzwa, wakiacha nyuma watu 5,000 wakiwa wamekufa na jiji lililoharibiwa.
1999 Mei – Kusitisha mapigano kunakaribishwa kwa matumaini huko Freetown huku kukiwa na matumaini kwamba miaka nane ya vita vya wenyewe kwa wenyewe inaweza kumalizika hivi karibuni.
1999 Julai – Majuma sita ya mazungumzo katika mji mkuu wa Togo, Lome, yanasababisha makubaliano ya amani, ambayo waasi wanapokea nyadhifa serikalini na hakikisho kwa mba hawatashtakiwa kwa uhalifu wa kivita.
1999 Novemba / Desemba – Wanajeshi wa UN wawasili ili kusimamia makubaliano ya amani – lakini kiongozi mmoja wa waasi, Sam Bokari, anasema hawahitajiki. Wakati huo huo, wanajeshi wa Ecomog wanashambuliwa nje ya Freetown.
2000 Aprili / Mei – Vikosi vya UN vinashambuliwa mashariki mwa nchi, lakini makubwa zaidi yanawangoja wakati 50, kisha wanajeshi mia kadhaa wa UN wakitekwa nyara.
2000 Mei – Waasi wanakaribia Freetown; Wanajeshi wa Uingereza 800 watumwa Freetown kuwahamisha raia wa Uingereza na kusaidia kuuchukua uwanja wa ndege kwa walinda amani wa UN; kiongozi wa waasi Foday Sankoh akamatwa
2000 Agosti – Wanajeshi kumi na moja wa Uingereza wanachukuliwa mateka na kundi la waasi walioitwa West Side Boys.
2000 Septemba – Vikosi vya Uingereza vinafanya operesheni kuwaokoa mateka waliobaki wa Uingereza.
2001 Januari – Serikali yaahirisha uchaguzi wa urais na bunge – uliopangwa mnamo Februari na Machi – kwa sababu ya ukosefu wa usalama.
Machi 2001 – Vikosi vya UN kwa mara ya kwanza vinaanza kupelekwa kwa amani katika eneo linaloshikiliwa na waasi.
2001 Mei – Kupokonywa silaha kwa waasi kunaanza, na jeshi la Sierra Leone lililofunzwa Uingereza linaanza kupelekwa katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi.
2002 Januari – Vita vimetangazwa kuisha. Ujumbe wa UN unasema kunyang’anywa silaha wapiganaji 45,000 kumekamilika. Serikali, UN zinakubali kuanzisha mahakama ya uhalifu wa kivita.
2002 Mei – Kabbah apata ushindi mkubwa katika uchaguzi. Chama chake cha People’s Party kinapata wajumbe wengi bungeni.
2002 Julai – Wanajeshi wa Uingereza wondoka Sierra Leone baada ya misheni yao ya miaka miwili kusaidia kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe.
2003 Julai – Kiongozi wa waasi Foday Sankoh afariki kwa sababu za asili wakati akisubiri kesi ya uhalifu wa kivita.