Na Gerald Lwomile
Moshi
Wakulima wa Kata ya Kahe wilayani Moshi wamesema hivi sasa furaha yao imerejea na wanaweza kulima kwa mafanikio baada ya kufundishwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA na Taasisi ya Utafiti wa Miti Tanzania TAFORI mbinu za kupambana na mti vamizi wa Mrashia au Mgunga Taveta ambao umewasumbua kwa muda mrefu
Wakizungumza na SUAMEDIA hivi karibuni wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, wakulima Rothamon Mshana na Zahara Yusuph wamesema mti vamizi wa Mrashia ambao umeenea sana katika mashamba yao umekuwa ukiwaletea shida kwa kufunga na kuzui mazao mengine kuota.
Dkt. Charles Kilawe Mtafiti kutoka SUA wa tatu kutoka kulia akiwa na wakulima wa Kahe Moshi na wanafunzi wanaofanya utafiti wa namna ya kuondoa Mti vamizi wa Mrashia (Picha zote na Gerald Lwomile)
Wamesema mti huo pia una uwezo wa kuenea kwa haraka na miba yenye sumu kali imekuwa ni changamoto inayosababisha kilimo kukwama
Bw. Mshana mkulima kutoka Kitongoji cha Reli B, amesema elimu na teknolojia waliyofundishwa na wataalamu kutoka SUA na TAFORI kwa kiasi kikubwa imewasaidia na sasa wanaona mwanga mpya katika uzalishaji wa mazao ya chakula katika wilaya hiyo iliyokuwa inaelekea kutawaliwa na miti hiyo
Kwa sasa hivi ili tuweze kuendelea na mrashia uweze kutokomezwa katika maeneo yetu tunahitaji serikali ituunge mkono katika kutusaidia vitu kama miundombinu ya maji, kwa sababu ya hali ya mvua, katika kata yetu hatuwezi kuvuna bila kumwagilia, mashamba mengi ni mapori na changamoto inayojitokeza ni jinsi ya kuundoa mrashia ni ngumu” amesema Mshana
Sehemu ya Shamba la majaribio ambalo lilikuwa limetawaliwa na mti vamizi wa Mrashia likiwa imestawi mahindi
Naye Bibi Zahara Yusuph mkulima katika Kijiji cha Oliaha Kahe amesema kuwa baada ya kupata elimu na teknolojia kutoka kwa wataalamu wanaona kabisa mti huo vamizi umeondoka katika mashamba ya majaribio na kuwa kama watatumia mbinu hiyo ya kulima mara kwa mara basi upo uwezekano mkubwa wa kuzuia kuendelea kuenea kwa mti huo
Mafanikio tuliyoyapata baada ya kupata elimu tumeona kwa kwa kweli ile miti imeisha, kwa sababu lengo kuu ilikuwa ni kuondoa mrashia ambao ni mti vamizi na umetusumbua kwa muda mrefu” amesema Bibi Zahara
Akizungumzia mafanikio mbalimbali ambayo yamepatikana katika mradi huo unaojulikana kama ‘Wood Weeds’ Mtafiti na Msimamizi wa Mradi huo kutoka SUA Dkt. Charles Kilawe amesema kwa kushirikiana na wakulima wameona njia ya kupambana na mti huo wa Mrashia kwa kutekeleza kilimo cha mara kwa mara
Ili kupambana na mti huu wa Mrashia au kwa kitaalamu unaitwa ‘Prosopis Juliflora’ ni muhimu wakulima kulima kilimo cha mara kwa mara ambacho hakiruhusu wakulima kupumzisha mashamba, hii njia hatukuileta sisi watalaamu bali tulishirikiana na wananchi nao wakachagua nini cha kufanya ili kupambana na mmea huu” amesema Dkt. Kilawe
Mti wa Mrashi ukiwa umeenea kwa wingi katika eneo, na hii ndiyo hali halisi ya mti huu unapovamia katika eneo na kutoruhusu shughuli za kijamii kuendelea
Mti wa Mrashia ambao umeendelea kuenea kwa kasi katika mikoa mbalimbali unaonesha kutokea Amerika ya Kusini na kusambaa katika maeneo mbalimbali hadi ukanda wa Afrika Mashariki ambapo nchini Tanzania uliingia kutoka katika nchi ya Kenya na huenezwa kupitia wanyama, upepo na watu kuupanda pasipo kujua madhara yake.