SUA yapongezwa kwa kutatua changamoto ya malisho

Wafugaji Rungwe wanufaika

Na Catherine Ogessa

Rungwe

Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya imekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa kuona umuhimu wa kutatua changamoto ya malisho inayowakabili wafugaji wilayani humo kwa kupeleka mradi unaoleta ufumbuzi wa tatizo la Malisho.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rungwe Dkt, Lawrence Kibona akifungua semina (Picha na Gerald Lwomile)

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halimashauri ya Rungwe Dkt. Lawrence Kibona wakati akifungua Semina kwa wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wasindikaji pamoja na watendaji wa Halmashauri hiyo wanaoshughulikia masuala ya kilimo wilayani humo ambayo ilikuwa inalenga kujadili hali ya mazingira na rasilimali zilizopo, pamoja shughuli za uzalishaji zilizopo wilayani humo.

“Kwa hiyo nichukue fursa hii kuwashukuru sana kwa kazi ambayo mnaendelea nayo, huku sasa wanasema kituo cha SUA na hasa wafugaji na sio kwamba wakulima na wafugaji wanakosea kuita kituo cha SUA hapana hii ni kwa sababu ya ukaribu wa timu ya mradi inashirikiana na wataalamu na wakulima na wafugaji “ amesema Kibona

Amesema kuwa wa mradi huo utasaidia kuwakomboa wana Rungwe na hata kwa wale ambao wapo nje ya mradi huo kwani kituo hicho kimekuwa ni sehemu ya mafunzo kwa watu wengi kwani  wamekuwa wakifika kituoni hapo kwaajili ya kujifunza na kuona malisho hayo ambayo yamekuwa ni mkombozi kwa wafugaji wa wilaya hiyo.

Washiriki wa semina wakisikiliza maelezo kutoka kwa mtaalamu juu ya upandaji wa majani ya malisho kwa mifugo (Picha na Gerald Lwomile)

Katika hatua nyingine amewataka maafisa mifugo kuhakikisha taarifa mbalimbali zinazowahusu wakulima na wafugaji zinapatikana ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili kwani kituo hicho ni muhimu kwao katika kupata taarifa.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa kushirikiana na nchi za Kenya, Malawi, Afrika Kusini Ethiopia pamoja na Rwanda zinaendesha mradi wa Innov Africa ambao ni mradi bunifu za kiteknolojia, kitaasisi na huduma ugani ili kufanikisha kilimo endelevu mradi ukifadhiliwa na nchi za Umoja wa Ulaya

Awali akimkaribisha kwenye semina hiyo Prof. Joseph Hyela ambaye ni mtafiti katika mradi huo wa malisho na pia mtaalamu wa masuala ya uchumi Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA amesema kuwa miongoni mwa sababu ambazo zilichangia Rungwe kuchaguliwa kufanyika kwa mradi huo  ni kutokana na ukweli kuwa eneo hilo linawafugaji wengi lakini wanakabiliwa na uhaba wa malisho.

Prof. Joseph Hyela ambaye ni mtafiti katika mradi huo wa malisho akitoa taarifa juu ya maendeleo ya mradi (Picha na Gerald Lwomile)

“Kitu kingine ambacho tulianzisha hapa ni kituo cha elimu na habari ambayo Halmashauri ilitoa chumba lakini napenda kukwambia kwamba katika maoni yetu kituo hiki hakijafanya kazi ambayo tumeikusudia…. Wanakijiji hawajaweza kuunganishwa na kituo hicho na tunadhani hayo ni mapungufu makubwa nadhani hivi sasa wakulima wetu wana simu janja lakini hakuna mtu ambaye amejiunga kwenye kundi la kimtandao la mawasiliano ili kupata taarifa lakini wengi wamejiunga kwenye makundi ya Simba au Yanga” amesema Prof Hyela

Washiriki wa semina ya mradi wa malisho wakiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Dkt, Lawrence Kibona aliyevaa koti jeusi mstari wa mbele 

Related Posts

Next Post

Discussion about this post

RECOMMENDED