SUA yakabidhiwa eneo na majengo Katavi

Yatakiwa iharakishe kupata ithibati ili idahiri 2020-2021

Na Josephoine Malango

Katavi

Viongozi, Wananchi na wadau mbalimbali wa elimu na kilimo wamesema ujio wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Mkoani Katavi  ni fulsa ya mabadiliko  kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini  ingawa bado inatajwa katika takwimu za kitaifa  kuwa na  changamoto  ya udumavu na umasikini

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya ardhi na majengo ambayo yatatumika kuwa Kampasi ya Mizengo Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu Mh. Mizengo Pinda ambaye ndiye aliyekuwa mmiliki wa awali wa ardhi na majengo hayo aliyojengewa  na wahisani amesema kulikuwa na malengo mengi ya matumizi ya majengo lakini lengo la kuwa Chuo cha Kilimo limeakisi hasa maana halisi ya ukanda  wa eneo husika kwa kuwa wakazi wengi wanajishughulisha na kilimo,uvuvi na ufugaji

Waziri Mkuu Mstaafu  Mhe. Mizengo Pinda kushoto aliyekaa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Mhe. Joseph Warioba kulia aliyekaa wakiweka saini ya makubaliano ya kukabidhiwa majengo hayo kwa SUA ( Picha na Josephine Malango)

Ameongeza kuwa uwepo wa SUA katika eneo hilo,  majengo hayo yatatumika kwa nia pana kuliko walivyofikilia na kutakuwa na ongezeko la  fulsa za kimaendeleo na thamani ya mkoa kuelekea kuchangia pato la taifa na kutokomeza alichokiita laana kwa baadhi ya Mikoa ikiwemo Katavi kutajwa katika takwimu za taifa za umasikini, udumavu na utapiamlo huku kukiwa na uzalishaji mkubwa wa chakula

Kwa upande wake mgeni rasmi katika hafla hiyo Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mh. Joyce Ndalichako amewashukuru SUA  kwa kuwa wepesi kukubali ombi la kuwa na  Kampasi  hiyo na kutekeleza kwa haraka  na ameagiza Chuo kifanye haraka  taratibu za kupata ithibati kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili kiruhusiwe kuanza udahili  wa wanafunzi mwaka huu wa masomo 2020-2021

Naye Mkuu wa Chuo cha Sokoine cha Kilimo SUA Jaji Mkuu Mstaafu Joseph Sinde Warioba amesema tangu nchi kupata kwa Uhuru wakulima wadogo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali pamoja na uwepo wa sera hivyo kuanzishwa kwa Kampasi ya Mizengo Pinda kutasaidia wakulima wa maeneo hayo kulima kwa tija na kuondokana na kilimo Cha mazoea

Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA Prof. Raphael Chibunda aliyekaa kulia akiweka saini moja ya mikataba ya makubaliano (Picha na Josephine Malango)

Kwa upande wake Makamu mkuu wa Chuo cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda  amesema kampasi hiyo mpya  itatumika kama  kituo cha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa SUA  wanaosoma fani mbalimbali zikiwemo  zile za Usimamizi wa Wanyamapori na Menejimenti ya Utalii,Kilimo, Mifugo, Mazingira na Ualimu wa Sayansi

Akizungumzia  Kampasi hiiyo kupewa jina la  Mizengo Pinda,  Mwenyekiti wa Baraza la Chuo  Jaji Mkuu Mstaafu, Othuman Chande amesema mchakato ulifanyika kuanzia menejimenti na hatimaye yeye aliridhia  kwa niaba ya Baraza lengo likiwa ni heshima na kuenzi juhudi, uzalendo na moyo mkubwa upendo aliouonesha Mh. Mizengo Pinda katika upatikanaji wa Kampasi hiyo

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Joyce Ndalichako aliyekaa  katikati amevaa gauni akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali walioshiriki katika makabidhiano ya eneo na majengo (Picha na Josephine Malango)

Kwa upande wao wakuu wa Mikoa waliohudhuria hafla hiyo kutoka Mkoa wa  Mbeya, Songwe, Tabora na Kigoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Juma Homera, wamesema watakitumia Chuo hicho kama shoka kwa kuwa ni fulsa ya kimaendeleo kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na kibiashara

Related Posts

Next Post

Discussion about this post

RECOMMENDED