Pamoja na kuwa mmea hatari lakini Mrashia unaweza kutumika kuinua uchumi

Unaweza kuzalisha bidhaa kama vyakula, vinywaji, dawa za kusafishia maji na kutibu  magonjwa

Na Gerald Lwomile

Mwanga, Kilimanjaro

 Pamoja na mti vamizi wa Mrashia au Mgunga Taveta ambao kitaalamu unaitwa “Prosopis juliflora” kuwa na madhara makubwa kwa mazingira na maisha ya jamii, lakini kama wananchi watafundishwa namna endelevu ya kuishi na huu mti  unaweza kuwaletea faida za kiuchumi

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Bw. Thomas Apson akifungua warsha ya matumizi bora ya mmea wa Mrashia (Picha na Gerald Lwomile)

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Bw. Thomas Apson wakati akifungua warsha iliyowakutanisha watafiti na wananchi ambao wanaishi katika kijiji cha Lang’ata Bora Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa changamoto nyingi za mti wa Mrashia ikiwa ni pamoja na kuzuia uoto wa asili katika maeneo ambayo unaota na kusababisha ulemavu kwa watu wanaochomwa na mwiba wa mti huo lakini mti huo unaweza kutumika kwa manufaa ya kiuchumi katika eneo ambalo umeota kwani mti huo si rahisi kuundoa.

“Ndugu wananchi mimea vamizi ni kati ya tishio kubwa kwa bioanuai na maisha ya viumbe ulimwenguni, ifahamike kuwa mimea vamizi ina sifa ya kukua kwa haraka, kustahimili ukame, kukosa magonjwa, kustahili ukame na hivyo kupendwa na watu wengi bila kujua kuwa inamadhara makubwa kwa jamii …. Lakini pamoja na kuwepo kwa mti huu wenye madhara bado wananchi sasa wanaweza kupata fursa ya kuutumia mti huu kwa manufaa ya kiuchumi kama kuni, kutengeneza mkaa, bidhaa kama asali na biskuti” amesema Bw. Apson

Huu ni muonekano halisi wa mbegu za mmea vamizi wa Mrashia (Picha na Dkt. Kilawe)

Akizungumzia kuhusu mti huo Mkuu wa Mradi huo kutoka Chuo Kikuu cha Nottingham cha nchini Uingereza Dkt. Zinnia Gonzalez-Carranz amesema mradi huu unatoa angalizo kuhakikisha mti huu hauenei kwani pamoja na kuwepo kwa faida hizo bado hasara ni kubwa kama utaendelea kusambaa katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na hifadhi za wayanyama pori na malisho ya mifugo.

Dkt. Zinnia Gonzalez-Carranz akizungumza na washiriki wa warsha wilayani Mwanga (Picha na Gerald Lwomile)

Amesema kuwa mti huo licha ya kuwa na madhara kutoka na utafiti uliofanyika lakini unaweza kuzalisha bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyakula, vinywaji, dawa za kusafishia maji na kutibu  magonjwa  mbalimbali

Dr.Zinnia amesema mbegu za mti huo zina Protini kwa wingi na kuwa kutokana na hali hiyo zinafaa sana katika utengenezajia wa vyakula mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyakula vya mifugo, biskuti, jams, bia na hata aina nyingine za matumizi ikiwa ni pamoja na shampoo za kusafishia nyele

Muonekano wa mmea wa vamizi wa Mrashia ukiwa umetengeneza umbo la mwamvuli (Picha na Dkt. Kilawe)

Akizungumzia utafiti waliofanya katika eneo la Kahe wilayani Moshi na Bwawa la Nyumba ya Mungu wilayani Mwanga Mtafiti kutoka Ndaki ya Misitu, Wanyapori na Utalii, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Dkt.  Charles Kilawe amesema katika utafiti wao waligundua kuwa  hasara ziletwazo na  mti huo ni kubwa kuliko faida.

Hata hivyo, amesema kwa maneneo ambayo tayari yamevamiwa kwa wingi, mti huo unaweza kutumika kutatua changamoto za kijamii ikiwepo ukosefu wa maji safi ya kunywa, nishati ya kuni,malisho ya mifugo na kuboresha maisha kwa kupitia miradi ya ufugaji nyuki.

“Mrashia  umenea sana katika maeneo ya Kahe Moshi vijijini, Ngorika Simanjiro, na Lang’ata Bora wilaya ya Mwanga. Mmea huu kama tulivyoona una faida nyingi faida za kuni, mkaa na kuvuli lakini mti huu unaweza kusababisha madhara makubwa na hasa mtu anapochomwa na ule mwiba wake, kuvamia makazi kwa hiyo kwa sababu una faida na hasara kubwa tunahitajika kujifunza kuishi na mti huu na kusababisha usiendelee kuenea” amesemna Dkt. Kilawe

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Bw. Thomas Apson aliyevaa shati jeupe katikati waliokaa akiwa katika picha ya pamoja na watafiti na wananchi ambao eneo lao la Lang’ata Bora limethirika na mmea wa Mrashia (Picha na Gerald Lwomile)

Naye Mkuu wa Mradi huo hapa nchini Prof. George Kajembe kutoka SUA amesema wananchi wanaoishi na mti huu katika maeneo yao wanayo fursa ya kuutumia kwa ajili ya shughuli za kiuchumi lakini itakuwa kosa kubwa kama wataendelea kuupanda katika maeneo mengine kwani unatabia ya kuharibu mazingira

Warsha hii ni moja ya zao la mradi wenye lengo kuu la kufanya “Utafiti wa matumizi bora ya mmea vamizi aina ya Mrashia ili kuboresha mazingira na maisha ya jamii zilizoathirika.

Mradi huu unafadhiliwa na Mfuko wa Utafiti wa Changamoto za Dunia wa Uingereza (GCRF, Uingereza) na kutekelezwa kwa pamoja na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Nottingham kilichopo Uingereza, Chuo Kikuu cha Nairobi Kenya, na Taasisi ya kusimamia misitu ya Mexico.

Mmea wa Mrashia ukiwa umefunga eneo kubwa ambalo linatumika kwa kilimo (Picha na Dkt. Kilawe)

Related Posts

Next Post

Discussion about this post

RECOMMENDED