Na Josephoine Malango
Katavi
Viongozi, Wananchi na wadau mbalimbali wa elimu na kilimo wamesema ujio wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Mkoani Katavi ni fulsa ya mabadiliko kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini ingawa bado inatajwa katika takwimu za kitaifa kuwa na changamoto ya udumavu na umasikini
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya ardhi na majengo ambayo yatatumika kuwa Kampasi ya Mizengo Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu Mh. Mizengo Pinda ambaye ndiye aliyekuwa mmiliki wa awali wa ardhi na majengo hayo aliyojengewa na wahisani amesema kulikuwa na malengo mengi ya matumizi ya majengo lakini lengo la kuwa Chuo cha Kilimo limeakisi hasa maana halisi ya ukanda wa eneo husika kwa kuwa wakazi wengi wanajishughulisha na kilimo,uvuvi na ufugaji
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda kushoto aliyekaa na Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Mhe. Joseph Warioba kulia aliyekaa wakiweka saini ya makubaliano ya kukabidhiwa majengo hayo kwa SUA ( Picha na Josephine Malango)
Ameongeza kuwa uwepo wa SUA katika eneo hilo, majengo hayo yatatumika kwa nia pana kuliko walivyofikilia na kutakuwa na ongezeko la fulsa za kimaendeleo na thamani ya mkoa kuelekea kuchangia pato la taifa na kutokomeza alichokiita laana kwa baadhi ya Mikoa ikiwemo Katavi kutajwa katika takwimu za taifa za umasikini, udumavu na utapiamlo huku kukiwa na uzalishaji mkubwa wa chakula
Kwa upande wake mgeni rasmi katika hafla hiyo Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mh. Joyce Ndalichako amewashukuru SUA kwa kuwa wepesi kukubali ombi la kuwa na Kampasi hiyo na kutekeleza kwa haraka na ameagiza Chuo kifanye haraka taratibu za kupata ithibati kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ili kiruhusiwe kuanza udahili wa wanafunzi mwaka huu wa masomo 2020-2021
Naye Mkuu wa Chuo cha Sokoine cha Kilimo SUA Jaji Mkuu Mstaafu Joseph Sinde Warioba amesema tangu nchi kupata kwa Uhuru wakulima wadogo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali pamoja na uwepo wa sera hivyo kuanzishwa kwa Kampasi ya Mizengo Pinda kutasaidia wakulima wa maeneo hayo kulima kwa tija na kuondokana na kilimo Cha mazoea
Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA Prof. Raphael Chibunda aliyekaa kulia akiweka saini moja ya mikataba ya makubaliano (Picha na Josephine Malango)
Kwa upande wake Makamu mkuu wa Chuo cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda amesema kampasi hiyo mpya itatumika kama kituo cha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa SUA wanaosoma fani mbalimbali zikiwemo zile za Usimamizi wa Wanyamapori na Menejimenti ya Utalii,Kilimo, Mifugo, Mazingira na Ualimu wa Sayansi
Akizungumzia Kampasi hiiyo kupewa jina la Mizengo Pinda, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Jaji Mkuu Mstaafu, Othuman Chande amesema mchakato ulifanyika kuanzia menejimenti na hatimaye yeye aliridhia kwa niaba ya Baraza lengo likiwa ni heshima na kuenzi juhudi, uzalendo na moyo mkubwa upendo aliouonesha Mh. Mizengo Pinda katika upatikanaji wa Kampasi hiyo
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Joyce Ndalichako aliyekaa katikati amevaa gauni akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali walioshiriki katika makabidhiano ya eneo na majengo (Picha na Josephine Malango)
Kwa upande wao wakuu wa Mikoa waliohudhuria hafla hiyo kutoka Mkoa wa Mbeya, Songwe, Tabora na Kigoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Juma Homera, wamesema watakitumia Chuo hicho kama shoka kwa kuwa ni fulsa ya kimaendeleo kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na kibiashara