Na:Catherine Mangula Ogessa
Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Japhet Hasunga amewataka wadau wa kilimo hususani Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuwasaidia wakulima katika kuhakikisha wanaondokana na kilimo cha hasara na badala yake walime kilimo cha kibiashara ambacho kitawaletea tija katika uzalishaji.
Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Japhet Hasunga Akifungua Kongamano la Maonesho na Kilimo kwa mwaka 2019, linalofanyika katika Chuo Kikuu SUA, picha na Vedasto George
Akifungua Kongamano la Maonesho na Kilimo kwa mwaka 2019, linalofanyika katika Chuo Kikuu SUA, Waziri wa Kilimo amesema kuwa wakulima wengi nchini ambao ni zaidi ya asilimia 80 wamekuwa wakilima kilimo cha hasara na sio cha kibiashara na kimsingi kimekuwa hakiwaletei tija
Aidha amefafanua kuwa wakulima wamekuwa wakitumia gharama kubwa katika kilimo ikiwa ni pamoja na muda wao wa kazi wanazozifanya lakini ajabu wamekuwa hawahesabu kama ni gharama kwa vile wamekuwa wakifanya wenyewe huku uhalisia ukiwa ni gharama na ni wazi kuwa kama wageujumuisha muda huo baada ya kuuza mazao watakuwa wamepata hasara badala ya kupata faida.
Kutokana na hali hiyo Mhe. Hasunga amewataka wadau hao kuangalia namna ambavyo wanaweza kuwasaidia wakulima ili kilimo kiwe na tija kwa kuhakikisha wanatumia zana, mbengu bora, maarifa bora pamoja wataalamu wa kilimo.
Katika hatua nyingine Waziri wa Kilimo amewataka washiriki wa kongamano hilo baada ya kukamilika kuangalia namna ambavyo wataishauri Serikali katika kuhakikisha ifikapo 2025 Tanzania inafikia katika Uchumi wa kati , kwani amelitaja kuwa Kongamano hilo ni muhimu katika kuishauri Serikali.
Mbali na hayo amekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa namna ambavyo kwa kimeleta mabadiliko kwa kuwa na mashamba darasa ambayo sio tu kwamba yatawasaidia wanafunzi kuwa wazuri zaidi mara wanapohitimu masomo yao kwa njia ya vitendo lakini pia yatawapa fursa wakulima kufika kujifunza.
Aidha amsema ni muhimu kutafuta teknolojia ambazo zitarahisisha shughuli za kilimo kwa vile hivi sasa kinakuwa ni kilimo kinachotumia nguvu nyingi na wakulima kukiona ni adhabu na badala yake watafute teknolojia ambazo zitawafanya wakulima kuweza kufurahia kujishughulisha na kilimo ili waweza kupata mazao yenye tija .
Kongamano ambalo linawashirikisha SUA, Watafiti, Watunga Sera, Mafisa Ugani pamoja na wakulima ambapo kaulimbiu ni “KUELEKEA TANZANIA YA UCHUMI WA KATI NA VIWANDA:JUKUMU LA MICHANGO YA WADAU WA SEKTA YA KILIMO NA MIFUGO”.