Watafiti na Wanasayansi katika masuala ya Kilimo wanayo nafasi kubwa katika kuwezesha utungwaji wa Sheria Kilimo na kanuni zitakazowezesha kusimamia sekta ya kilimo ili kuweza kukifanya kilimo kutoa tija inayotakiwa kwa maendeleo ya Wakulima na nchi kwa ujumla.
Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi MoCU Utawala na fedha Prof. Fredy Kilima(Kulia) Akimkabidhi zawadi ya Kinyago Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe mara baada ya kufungua Mkutano huo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe wakati akifungua Mkutano wa Kisayansi wa Mwaka wa wataalamu wa Uchumi kilimo Tanzania AGREST Jijini Dodoma mkutano ambao unakutanisha Wataalamu hao zaidi ya 100 kutoka nchi nzima.
Mhe. Bashe amesema kwa Mara ya kwanza Tanzania kupitia Wizara yake ya Kilimo inatengeneza sheria mahususi kwaajili ya kusimamia Sekta ya kilimo nchini badala ya kutegemea sheria za Bodi za mazao na sheria zingine mbili ambazo zinatarajiwa kukamilika mwakani.
Naibu Waziri huyo amesema unapozungumzia sekta ya kilimo na maendeleo yake huwezi kuwaweka pembeni wataalamu hao wa uchumi kilimo hivyo atawaalika rasmi ofisini kwake ili waweze kutoa mapendekezo yao kuhusu sheria hiyo ya Kilimo ili iweze kuketa tija kwa Taifa.
Katika hatua nyingine Mhe. Bashe amewataka wataalamu hao wa Uchumi Kilimo kuangalia utekelezaji wa ASDP II ili iweze kutimiza malengo yake hasa baada ya ASDP i kushindwa kufikia malengo yake.
“ Sote tunajua kuwa ASDP I haikufanya vizuri kwahiyo ASDP II inarekebisha makosa ya awali hivyo nyinyi kama wataalamu wa Uchumi Kilimo mtusaidie kuiangalia hii ili iweze kufikia malengo na matarajio ya Serikali na Wakulima wote” Alisisitiza Mhe. Bashe.
Akizungumzia Utafiti Mhe. Naibu waziri huyo amesema zipo tafiti nyingi zinafanyika nchini ambazo matokeo yake hayatekelezeki kwa wakulima vijijini huko hivyo ni vyema Watafiti wala kaenda teknolojia na mbinu ambazo ni rahisi na wakulima watakazoweza kuzitumia na kuboresha kilimo chao.
Mhe. Bashe ameongeza kuwa tafiti nyingi zinazofanywa kwa msaada wa wafadhili toka nje haziakisi mahitaji halisi ya Watanzania bali matakwa yao hivyo ni vyema watafiti wakaja na aina za teknolojia ambazo kweli zinahitajika na Wakulima wetu ili tafiti ilete tija badala ya kufanya tafiti zenye mlengo wa mfadhili pekee.
“Nawaahidi nitahakikisha nawaunganisha na wadau wowote wa maendeleo na wafadhili ambao wanakuja ofisini kwangu au ninaokutana nao ili mawazo yenu mazuri yaweze kufanyiwa utafiti na kuboresha Sekta hii muhimu kwa taifa letu ambayo inatoa ajira nyingi zaidi” Alisisitiza Naibu waziri huyo Mhe. Hussein Bashe.
Amesema anaamini Mkutano huo wa Kisayansi wa Mwaka wa Wataalamu wa Uchumi Kilimo AGREST utakuja na mapendekezo ambayo yatasaidia Serikali katika maendeleo ya Kilimo na Ushirika.
Awali akiongea kabla ya Kumkaribisha Amidi wa Shule kuu ya Uchumi Kilimo na stadi za bishara kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano huo Mwenyekiti wa AGREST Dkt. Elibariki Msuya amesema katika mkutano huo wa 11 utahusisha Wanafunzi,Wataalamu, Watafiti, Maafisa wa Serikali na mashirika yasiyo ya Kiserikali ambapo jumla ya machapisho ya kisayansi 44 yatawaailishwa na kujadiliwa.
Dkt. Msuya amesema Mkutano huo unatoa fursa kwa wadau na Wanachama kubadilishana mawazo kuhusu jitihada mbalimbali za maendeleo ya kilimo zinazofanywa na wadau mbalimbali juu ya mabadiliko ya kimazingira na kujifunza kutoka kwa wengine.
Mwenyekiti huyo wa AGREST amesema Mkuatano huo wa Kisayansi utatoa fursa kwa Wanasayansi na Wataalamu wa fani ya Uchumi kilimo wachanga kujenga uzoefu wa namna ya kuandaa na kuwasilisha kazi za Kisayansi.
“ Mhe. Mgeni Rasmi Mbiu ya Mkutano wetu huu ni Mapinduzi ya nne ya Viwanda na mchango wake kwenye maendeleo ya sekta ya Kilimo na usindikaji “ Alisema Dkt. Msuya.
Amesema mapinduzi ya nne ya Viwanda yatachangia mabadiliko ya Kilimo na usindikaji wa Mazao ya kilimo lakini pia yataleta fursa mpya na changamoto katika kilimo barani Afrika.
Katika mkutano huo Chama hicho cha wataalamu wa Uchumi Kilimo na biashara za kilimo wamempatia Naibu waziri huyo wa Kilimo Mhe. Bashe zawadi mbalimbali kama shukrani na ukumbisho kwake kutoka kwa Wana AGREST na zawadi zingine.
Naibu waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe akisisitiza jambo mara baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa 11 wa AGREST jijini Dodoma na kulia ni Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo Utawala na fedha wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi MoCU Prof. Fredy Kilima.
Washiriki wa Mkutano huo wakimsikiliza Naibu Waziri wa Kilimo (hayupo pichanni) wakati akifungua mkutano huo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Uchumi Kilimo na Bishara za Kilimo AGREST Dkt. Elibariki Msuya akitoa neno la utangulizi kabla ya Mgeni rasmi kufungua mkutano huo wa 11 wa Chama hicho.
Washiriki na wanachama wa AGREST wakiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe jijini Dodoma kwenye ukumbi wa St. Gasper
Picha zote na Calvin E Gwabara.
SOMA PIA KUPITIA LINK HAPA CHINI